MAANA NA AINA ZA TAMTHILIYA
Na Mwl. Kagita
TAMTHILIYA
Kwa
kuanza na maana ya tamthiliya imeelezwa na wataalamu mbalimbali kwa namna
tofautitofauti kulingana na vigezo walivyovizingatia.
Mwenda
Ntarangwi, (2002:169) anaeleza kuwa, neno tamthilia limetokana na kitendo
“mithilisha” ambacho maana yake ni kufananisha au kumithilisha hali ya maisha
fulani kwa vitendo. Akahitimisha kwa kusema tamthilia ni maigizo ya matukio au
visa fulani kwa uhalisi wake kwa ajili ya kuyasawili maudhui au maelezo fulani.
Ubora unaojitokeza katika maana hii ni kuzingatia vipengele vya uigizaji,
tukio, suala la kuhusianisha na jamii na kubeba maudhi Fulani.
Udhaifu
wa maana hii ni kutozingatia kipengele cha ubunifu pia hakueleza hayo maigizo
yanatakiwa yawe ya namna gani ili yaitwe tamthiliya.
Wamitila, (2002:7) ameeleza kuwa, neno tamthiliya kwa upana wake linatumiwa
kujumuisha maneno drama na play ya
Kiingereza. Kwa hiyo, tamthiliya ni utungo unaoandikwa kwa mtindo wa
mazungumzo. Ubora wa fasili hii imezingatia kipengele cha mazungumzo ambacho ni
kipengele muhimu katika tamthiliya.
Udhaifu
wa fasili hii kwanza amechanganya dhana ya tamthiliya na drama ambazo ni dhana
mbili tofauti. Kwani tamthiliya msisitizo wake upo katika maandishi lakini
drama msisitizo wake upo katika uigizwaji jukwaani. Pia si kila mazungumzo ni tamthiliya.
Kigezo cha mazungumzo pekee hakitoshi kuamua utungo fulani kuwa ni tamthiliya.
Penina Mlama, (1983:203) akirejelewa na
Mulokozi, (1996) anasema tamthiliya ni sanaa za maonyesho; sanaa ambayo
huwasilishwa ana kwa ana, tukio fulani kwa hadhira kutumia usanii wa
kiutendaji. Katika fasili hii Mlama amezingatia vipengele vya sanaa,
uonyeshaji, hadhira, utendaji na tukio.
Udhaifu
wa maana hii ni kuwa si lazima tamthiliya iigizwe jukwaani; vilevile fanani na
hadhira si lazima wawe ana kwa ana. Mfano katika tamthiliya ya “Kivuli
Kinaishi” “Ngoma ya Ng’wanamalundi”, “Lina Ubani” na nyinginezo, fanani na
hadhira hawapo ana kwa ana.
Udhaifu
wa fasili hii Mlama hakuweka wazi urefu huu kuwa ni urefu wa kurasa nyingi au
urefu wa tukio linalosimuliwa. Pia si kila hadithi inayosimuliwa jukwaani ni
tamthiliya. Kwani hata misikitini na makanisani wahubiri husimama juu ya
mimbari kuhutubia waumini wao. Je, hiyo ni tamthiliya? Jawabu ni kuwa hiyo siyo
tamthiliya.
Sanjari
na hao Mulokozi, (1999:188) anasema kuwa tamthiliya au drama ni fani ya fasihi
iliyokusudiwa kutendwa jukwaani kwa ajili ya hadhira fulani. Ubora unaopatikana
katika maana hii ni kwa kuwa imezingatia utendaji, jukwaa, hadhira, kusudio na
fani inayotendwa. Kwa upande wa udhaifu, maana hiiimechanganya dhana ya
tamthiliya na drama. Lakini kwa kiasi kikubwa maana hii inaonekana kukidhi
vigezo vingi.
Tunakubaliana
na Mulokozi (1996) kuwa sifa walizotoa Mlama na Balisidya kuwa tamthiliya huwa
na sifa za kawaida za sanaa za maonyesho. Sifa hizo ni dhana inayotendeka,
mtendaji, uwanja wa kutendea, na watazamaji. Hivyo sifa hizi hazitoshi
kupambanua sanaa ya maonesho; kwa sababu kuna matendo mengine ya kijamii ambayo
yana sifa hizo. Mfano matambiko, hotuba zinazotolewa na watu mbalimbali.
Mulokozi alisema sanaa za maonesho ni tukio lenye sifa saba ambazo ni dhana
inayotendwa, uwanja wa kutendea, watendaji, hadhira, kusudio la kisanaa,
muktadha wa kisanaa na ubunifu.
Kwa
jumla tunaifasili tamthiliya kuwa ni utanzu wa fasihi unaotumia lugha ya
majibizano yenye ubunifu wa hali ya juu ikiwa haina msisitizo wa uwasilishaji
wake jukwaaani ili kufikishalengo mahususi
kwa hadhira iliyokusudiwa kwa njia iliyoandikwa au isiyoandikwa.
Kutokana
na kuwa dhana ya tamthiliya inachanganywa na maana ya drama ni vyema tuelezee maana
ya drama. Kwa mujibu wa Wamitila, (2003:36) anasema kwamba drama ni aina ya
utanzu wa fasihi ambao kimsingi hudhamiriwa kuigizwa mbele ya hadira. Inaweza
kuwa imeandikwa au la.
Kwa
jumla dhana ya drama inarejelea utungo wa kisanaa unaotumia lugha ya majibizano
na matendo yenye ubunifu wa hali ya juu yanayotendwa jukwaani mbele ya hadhira
ili kufikisha lengo mahususi kwa hadhira iliyokusudiwa.
SIFA ZA
TAMTHILIYA
·
Utoshelevu Kimuundo. Tamthiliya nzuri
huwa na sehemu tatu muhimu: Mwanzo, Katikati na Mwisho. Sehemu zake
zinatazamiwa kuingiliana, kujengana na kukamilishana.
·
Tamthiliya huwa na lengo. Katika zama za
Aristotle, kwa mfano, tanzia ziliwajibika kuzindua hofu na huruma.
·
Vitendo vyote vinavyofanyika katika
tamthiliya vinapaswa kuchangia katika ufanisi wa dhamira za mtunzi.
·
Kifani, tamthiliya hutumia mbinu za
kisanii zinazowishi wasomaji au watazamaji kuendelea kusoma au kutazamia
matokeo ya matendo yanayoigwa. Mbinu hizo ni pamoja na jazanda, kejeli,
ritifaa, tashbihi, tashihisi na uzungumzi nafsia.
·
Wasanii bora wa tamthiliya ni wale
wanaotunga tamthiliya zinazozungumzia kadhia zinazoweza kutimia katika maisha
ya binadamu.
UHALISIA
MAZINGAOMBWE
Uhalisia
mazingaombwe ni dhana ambayo imeanza kutumika
miaka ya 1920, ambapo mjerumani Franz Roh ndiye aliyevumbua matumizi ya Magical realism mnamo mwaka 1925 ili
kuelezea kazi ya mtindo wa ulaya enzi hizo. Roh alilibuni neno hili ili kuelezea michoro iliyo na uhalisi kama wa
picha na kamera. Michoro hiyo ilichanganya mambo ya uhalisi na yasiyokuwa na
uhalisi.Baadaye dhana hii ya Uhalisia Mazingaombwe ilitumiwa na Arturo Urslar kutoka Venezuela
alipokuwa anahakiki kazi mbalimbali za wanafasihi wa Marekani ya Kusini
waliokuwa wanatumia mtindo huu katika kazi zao. Baadaye Uhalisia Mazingaombwe
ulianza kutumika kama nadharia ya uchambuzi wa kazi za kifasihi.
Katika
fasihi ya Kiswahili wataalamu mbalimbali wanaeleza kuwa, Uhalisia mazingaombwe
ni mtindo uliokuwa ukitumika muda mrefu hata kabla ya taaluma ya uandishi.
Mtindo huu ulitumika katika fasihi simulizi na baadae ukatumika katika fasihi
andishi. Wanaotumia mtindo huu katika fasihi andishi wanarudia au kufufua kitu
ambacho kilikuwepo zamani. (Senkoro2007:11)
Dhana
ya uhalisia mazingaombwe imefasiliwa na wataalamu mbalimbali kama ifuatavyo;
Wamitila
(2003 a:274), anaeleza kuwa ni mtindo wenye sifa za kuyaelezea matukio ya
kifantasia, kiajabu, au kiuchawi kwa
namna ya moja kwa moja inayofanya yaonekane ya kawaida tu.
Faustine,
S akimrejelea Methew, S. (1999:267) anasema, Uhalisia Mazingaombwe ni yale
mambo ambayo hutokea pale ambapo mandhari na matukio halisi yanavamiwa na jambo
ambalo ni la ajabu mno na ni vigumu kuaminika.
Kwa
jumla, fasili zote zimegusia uhalisia mazingaombwe kama mbinu ambayo mambo ya
ajabuajabu, uchawi, na yasiyo ya kawaida kutokea sambamba na yale yaliyozoeleka
katika ulimwengu halisi tuujuao na kuuishi. Katika mbinu hii mazingaombwe
hujitokeza kupitia wahusika, mandhari,
motifu ya kisafari na matukio kama misingi mikuu ya uchambuzi wa nadharia hii
ambamo ndani yake kumefichwa taswira, ishara na sitiari zinazohusiana na maisha ili kufikisha ujumbe
uliokusudiwa kwa jamii.
Uhalisia
Mazingaombwe huwa na sifa kama vile; matukio ya kustaajabisha, motifu ya
kisafari, matumizi ya taswira na ishara kwa kiasi kikubwa ambayo hujengwa
kutokana na matukio, wahusika na
mandhari. Vilevile mbinu hii hutumika ili kuwakilisha kitu au jambo fulani.
Athari ya mbinu hii
inajitokeza katika kazi za waandishi wa mwanzo wa fasihi ya Kiswahili hasa
Shaaban Robert na kazi za “Kusadikika” na “Adili na nduguze”.Katika kazi hizi
masuala ya safari yanajitokeza kwa kiasi kikubwa, safari siyo jambo la ajabu
katika ulimwengu halisi wa maisha japo baadhi ya masaibu yaliyowafika wasafiri
waliomo katika kazi hizi ni vigumu kuyaamini katika ulimwengu halisi kwani
yamefungamanishwa na uajabuajabu mno. Huo uajabu ndiyo uliofanya kazi hizi na
zilizofuatia baadaye kama “Babu
alipofufuka” na “Mzingile”
kudaiwa zimetumia mbinu za uhalisia mazingaombwe katika kueleza ukweli na hali
ya maisha ya jamii walizokusudia waandishi wa kazi hizo
Udhaifu wa uhaalisia mazingaombwe
katika kazi ya fasihi.
Kuhusisha wahusika
wakuu walio na akili zisizo timamu, mwingiliano-matini uliopindukia na
utambulisho wenye kutetereka.
Umefungwa kwa minyororo
ya lugha, na hivyo basi hauwezi kuondoa udhaifu wa lugha katika kuweza
kuwakilisha hali halisi kikamilifu.
UCHOTARAISHAJI
Uchotaraishaji au fasihi ya
Kiswahili ya majaribio, ni fasihi ambayo
imechota vipengele vya fasihi simulizi ya Kiswahili na kuviweka katika fasihi
andishi ya Kiswahili, kwa lengo la kuleta vionjo vipya katika fasihi ya
kiafrika. Dhana ya uchotaraishaji inarejelea kufufua fasihi asili ya Kiswahili
kwa kutumia mbinu na vipengele vya fasihi simulizi katika tanzu za fashi andishi kama vile riwaya, ushairi na
tamthiliya.
Uchotaraishaji ulifanywa mwanzoni hapa Tanzania na waandishi maarufu wa
tamthiliya ya kiswahili kama vile, Ebrahim Hussein na Penina Muhando. Ebrahim Hussein alitumia mbinu hii katika
tamthiliya yake ya Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi, na Penina Muhando katika
tamthiliya yake ya Lina Ubani.
Baadhi ya sifa za uchotaraishaji ni;
Mtambaji, sifa hii hujitokeza katika fasihi ya Kiswahili
ya majaribio. Katika tamthiliya ya Lina
Ubani, mbinu hii ya utambaji imejidhihirisha, pale ambapo mtambaji
anasimulia hadithi ya Bibi.
Mtambaji: Paukwa
Hadhira : Pakawa
Mtambaji: Hapo zamani za siku hizi, palitokea huyo Bibi kama
mnavyomuona...............…(uk
2)
Matumizi ya taswira na ishara, mbinu
hii hutumiwa katika fasihi simulizi kuwasilisha wazo kwa hadhira iliyokusudiwa.
Dhana hii imetumiwa katika tamthiliya ya Lina
Ubani, ambapo mwandishi ametumia taswira ya zimwi, kuashiria utawala wa mabavu wa aliyekuwa rais wa Uganda Nduli Idd Amin, kama anavyosema Mtambaji;
.......Mwisho Zimwi likaamua fujo kuzifanya asubuhi na mapema,ukingoni
mwa msitu lilisimama,likapiga makelele kuteremsha ardhi.(uk 18).
Wahusika, na majina, katika tamthiliya ya Lina Ubani, wahusika waliotumiwa ni Binadamu wenye majina halisi ya
kiafrika, wahusika kama Bibi, Huila, Mwana Hego, Mota pia Mhusika Zimwi ambaye
katika jamii za kiafrika huashiria ubaya.
Mwingiliano wa tanzu, (utomeleaji).
Mbinu hii imejitokeza katika fasihi
simulizi ambapo vipengele vya fasihi simulizi
huingiliana katika utumizi.
Katika tamthiliya ya Lina Ubani,
kuna hadithi ndani ya tamthiliya pia matumizi ya wimbo ambao umeambatanishwa na
utambaji. Bibi amekaa analia kwa kuimba na kuomboleza, licha ya hivyo wimbo
wenyewe uko katika lugha ya jadi ya Kiafrika na una tafsiri yake kwa Kiswahili.
Ing’oma ii
sikuidaha doo ae Ngoma hii
siwezi Oooh!
Woi doo ae aya
Nimemwitunda dya
mele do Nisimame juu ya
mlima wa Mele
Ninange main a
baba do Niite baba
na mama (uk 1-3)
Mianzo na Miisho ya kifomula, hii ni sifa ya kimsingi katika hadithi za
fasihi simulizi ya kiafrika ambapo fanani huanza kuhadithia kwa kuweka viashirio
maalumu kwa mfano, fanani husema ;
Fanani :Paukwa
Hadhira:Pakawa
Katika tamthiliya ya Lina Ubani,mwandishi ameanza kwa kuelezea hadithi yake kwa
mianzo kama ya hadithi ya fasihi
simulizi,kwa mfano
Mtambaji :
Paukwa
Hadhira: Pakawa
Mtambaji:
Hapo zamani za siku
hizi…………………(uk-2). Mwishoni Mtambaji
amemalizia kwa kitendawili ambacho anaomba hadhira impe mji ili kumalizia
hadithi yake mfano Mtambaji:
Akaa!
Mwenyewe
bibi kajifia
Hadithi
hakumalizia
Mkitaka
nimalizie mimi
Nipeni mji
Lakini mji
wenyewe
Usiwe na
uvundo
Kwa sababu
ubani wa uvundo
Mie siujui.
TANZIA-RAMSA
Ni tamthiliya
inayochanganya vipengele vya tanzia na ramsa, hutumiwa sawa na tamthiliya za
kibwege - hii ni tamthiliya ambayo inaonyesha kwamba kicheko au furaha ndiyo
jibu pekee la maisha kwa watu ambao hawana imani na maisha ambayo kwayo misingi
thabiti ya maisha imeondolewa. Mfano tamthiliya ya Amezidi ya S.A Mohamedi
Tanzia-ramsa ni
tamthilia ambayo huonyesha mabadiliko ya aina fulani yanayogeuza mwelekeo wa
matukio ya kitanzia na kuufanya kuwa tofauti au wa kufurahisha. Hali hii
inaweza kupatikana kwa kuwepo kwa hasidi au mui anayetubu na kuyajutia makosa
au msimamo wake au kuwepo kwa mandhari ya kiulimbwende.
Kimsingi,
tanzia-ramsa ni tanzia inayoishia kwa furaha. Kinyume chake ni futuhi zimbwe. Dhana hii inaakisi kwa
kiasi kikubwa baadhi ya mitazamo ya kidhanaishi ya fasihi ambapo ushujaa na
tanzia havijitokezi katika hali ya kawaida kama vilivyozoeleka.
Hali hii
inadhihirika katika tamthiliya kama vile ‘The
Cherry Orchard’ (Anton Chekhov, 1904), ‘The
Winter’s Tale’ (William Shakespeare, 1611).
FUTUHI/KOMEDIA
(COMEDY)
Futuhi au
komedia ni utungo ambao unachekesha na kuchangamsha. Tamthiliya ya aina hii
inaweza kusawiria picha halisi katika maisha
kwa undani ikitumia dhihaka na kejeli kwa kuchekesha. Futuhi huficha
ukali wa masuto kadri inavyoendelea kuburudisha hadhira yake.
Futuhi hulenga
kurekebisha tabia zinazozidhihaki au zinazozicheka. Kusema futuhi inafurahisha
haina maana kuwa dhamira yake haina uzito, kwani huzungumzia masuala ya kijamii,
kisiasa na kiuchumi kwa njia ya kuchekesha. Futuhi huweza kuwa na sifa
zinazotofautiana – jambo ambalo hutumiwa kama kigezo cha kuainisha aina
mbalimbali. Lakini vyovyote iwavyo, futuhi hujikwepesha na masuala ya kutia
hofu au kushtua.
Athari ya futuhi
(kuchekesha) hutokana na matendo, mienendo ya wahusika na hitilafu au ila za
kuingiliana kwa kiusemi. Futuhi huwa na viwango mbalimbali vya kuchekesha.
Kwanza, kuna
kiwango hafifu (duni) ambacho huhusishwa na futuhi ya chini. Kuna baadhi ya
kazi ambapo kiwango cha kuchekesha huwa kigumu kutambulikana na huhitaji
utambuzi mpevu. Hii ni sifa ya aina ya futuhi iitwayo Futuhi ya Juu.
Aina zingine ni
pamoja na, futuhi ya kikanivali, kitashtiti, maadili, mawazo, ucheshi na
zimbwe. Mifano mizuri ya futuhi ni ‘Aliyeonja
Pepo’ (Topan, F.), ‘Usaliti Mjini’
(Imbuga, F.), Twelfth Night
(Shakespeare, W.), Importance of Being
Earnest (Wilde Oscar), Mkaguzi Mkuu
wa Serikali (Gogol, Nikolai), The
Lion and the Jewel (Soyinka, W.) na ‘Masaibu
ya Ndugu Jero’ (Soyinka, W.).
MELODRAMA
Katika zama za
urasimi, aina hii ilitumiwa kuelezea aina ya drama au tamthiliya iliyokuwa na
matumizi mengi ya uimbaji au nyimbo (melos). Kwa hiyo, melodrama ni dhana
inayotumiwa kuelezea aina ya tamthiliya ambayo imetawaliwa na uimbaji wa nyimbo.
Melodrama
inafanana sana na tanzia ingawa mara nyingi nguli wa melodrama humalizika na
ushindi, matokeo yake yanasisimua sana na mwendo wa msuko wake huwa ni wa
haraka haraka zaidi. Wahusika wake huvutia na kufurahisha lakini hawana sifa za
kishujaa.
Dhamira ya
melodrama huzungukia mvutano kati ya wema na uovu au ubaya. Miishio ya
tamthiliya hizi haina sifa ya mtakasohisia kama ilivyo na tanzia bali huwa ni
aina ya ushindi wa mhusika mwema. Mfano mzuri ni ‘The Begger’s Opera’ iliyotungwa na mwanatamthiliya wa Kiingereza
John Gay kunako 1728.
TANZIA-RAMSA
Ni tamthiliya
inayochanganya vipengele vya tanzia na ramsa, hutumiwa sawa na tamthiliya za
kibwege - hii ni tamthiliya ambayoinaonyesha kwamba kicheko au furaha ndiyo
jibu pekee la maisha kwa watu ambao hawana imani na maisha ambayo kwayo misingi
thabiti ya maisha imeondolewa. Mfano tamthiliya ya Amezidi ya S.A Mohamedi
Tanzia-ramsa ni
aina huonyesha mabadiliko ya aina fulani yanayogeuza mwelekeo wa matukio ya
kitanzia na kuufanya kuwa tofauti au wa kufurahisha. Hali hii inaweza
kupatikana kwa kuwepo kwa hasidi au mui anayetubu na kuyajutia makosa au
msimamo wake au kuwepo kwa mandhari ya kiulimbwende.
Kimsingi,
tanzia-ramsa ni tanzia inayoishia kwa furaha. Kinyume chake ni futuhi zimbwe. Dhana hii inaakisi kwa
kiasi kikubwa baadhi ya mitazamo ya kidhanaishi ya fasihi ambapo ushujaa na
tanzia havijitokezi katika hali ya kawaida kama vilivyozoeleka.
Hali hii
inadhihirika katika tamthiliya kama vile ‘The
Cherry Orchard’ (Anton Chekhov, 1904), ‘The
Winter’s Tale’ (William Shakespeare, 1611).
FUTUHI/KOMEDIA
(COMEDY)
Futuhi au
komedia ni utungo ambao unachekesha na kuchangamsha. Tamthiliya ya aina hii
inaweza kusawiria picha yakini katika maisha
kwa undani ikitumia dhihaka na kejeli kwa kuchekesha. Futuhi huficha
ukali wa masuto kadri inavyoendelea kuburudisha hadhira yake.
Futuhi hulenga
kurekebisha tabia inazozidhihaki au inazozicheka. Kusema futuhi inafurahisha
haina maana kuwa dhamira yake haina uzito. Futuhi huzungumzia masuala ya
kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa njia ya kuchekesha. Futuhi huweza kuwa na sifa
zinazotofautiana – jambo ambalo hutumiwa kama kigezo cha kuainisha aina
mbalimbali. Lakini vyovyote iwavyo, futuhi hujikwepesha na masuala ya kutia
hofu au kushtua.
Athari ya futuhi
(kuchekesha) hutokana na matendo, mienendo ya wahusika na hitilafu au ila za
kuingiliana kwa kiusemi. Futuhi huwa na viwango mbalimbali vya kuchekesha.
Kwanza, kuna
kiwango hafifu (duni) ambacho huhusishwa na futuhi ya chini. Kuna baadhi ya
kazi ambapo kiwango cha kuchekesha huwa kigumu kutambulikana na huhitaji
utambuzi mpevu. Hii ni sifa ya aina ya futuhi iitwayo Futuhi ya Juu.
Aina zingine ni
pamoja na, futuhi ya kikanivali, kitashtiti, maadili, mawazo, ucheshi na
zimbwe. Mifano mizuri ya futuhi ni ‘Aliyeonja
Pepo’ (Topan, F.), ‘Usaliti Mjini’
(Imbuga, F.), Twelfth Night
(Shakespeare, W.), Importance of Being
Earnest (Wilde Oscar), Mkaguzi Mkuu
wa Serikali (Gogol, Nikolai), The
Lion and the Jewel (Soyinka, W.) na ‘Masaibu
ya Ndugu Jero’ (Soyinka, W.).
MELODRAMA
Katika zama za
urasimi, aina hii ilitumiwa kuelezea aina ya drama au tamthiliya iliyokuwa na
matumizi mengi ya uimbaji au nyimbo (melos). Kwa hiyo, melodrama ni dhana
inayotumiwa kuelezea aina ya tamthiliya ambayo imetawaliwa na uimbaji wa
nyimbo.
Melodrama
inafanana sana na tanzia ingawa mara nyingi nguli wa melodrama humalizika na
ushindi, matokeo yake yanasisimua sana na mwendo wa msuko wake huwa ni wa
haraka haraka zaidi. Wahusika wake huvutia na kufurahisha lakini hawana sifa za
kishujaa.
Dhamira ya
melodrama huzungukia mvutano kati ya wema na uovu au ubaya. Miishio ya
tamthiliya hizi haina sifa ya mtakasohisia kama ilivyo na tanzia bali huwa ni
aina ya ushindi wa mhusika mwema. Mfano mzuri ni ‘The Begger’s Opera’ iliyotungwa na mwanatamthiliya wa Kiingereza
John Gay kunako 1728.
2.
RAMSA/KOMEDI
Ni tamthiliya ambayo inachangamsha na huishia
kwa kufurahisha na ni ya vichekesho, hii haina maana kwamba haina maudhui
mazito ndani yake.
Inashughulikia mambo yale yale yanayoweza
kushughulikiwa na tanzia. Mfano masuala ya unafiki,uzembe, wivu, hivyo
inayashughulikia kwa namna tofauti na tanzia
Udhati
wa ramsa si kwamba usanii humalizika katika kicheko/furaha zaidi ni kuishia
mhusika mkuu kufanikiwa
Shujaa
wa kiramsa
·
Si lazima awe mtu maalum/mbabe au
shujaa, anaweza kuwa mtu wa kawaida
·
Mhusika wa ramsa lazima awe mtu wa
wastani chini ya wastani, awe ni mtu ambaye hatarajiwi kujitokeza na mtu wa
nasaba duni na matendo yake yawe ya ucheshi
·
Ni lazima awe mtu ambaye akifanikiwa
wasomaji au watazamaji watafurahi
Uhusika katika ramsa
·
Ramsa inawahusu watu wa kawaida kuliko
ilivyo tanzia
·
Inawahusu watu wa kipato cha kati na cha
chini
·
Dhamira zote huelekezwa kwa watu wa
kipato cha chini na duni. Mfano walalahoi
SIFA ZA RAMSA
·
Sharti ivutie akili na siyo hisia
·
Ni lazima kuwa na matendo bila kufikiria
hii itapelekea msomaji au mtazamaji kujua kwamba wahusika hawa hawana akili
·
Lazima iwe na hali ya utu (ikitukumbusha
ubinadamu wetu)
·
Sharti iwe na mila na desturi ambazo
hadhira inazifahamu toka katika jamii yake
·
Hadhira isiogope au kupata uchungu kwa
sababu hii sio lengo lengo la ramsa
·
Wahusika wa ramsa hujaribu kuepuka
vikwazo ambavyo vimewekwa
·
Inaonyesha haja ya kuikomboa nafsi Mfano
wa ramsa ni kama vile Mfalme Juha.
MAREJELEO
Muhando,P. (1982), Lina Ubani, Dar
es Salaam University Press: Dar es Salaam.
Wamitila, K.W. (2003), Kichocheo cha
Fasihi Simulizi na Andishi. English press: Nairobi
Senkoro, F. E. M. K. (2006), Kioo cha
Lugha, Fasihi ya Kiswahili ya Majaribio; Juzuu namba (4) TUKI: Dar es
Salaam.
NB; Makosa ya kitahajia au kimaana yaliyojitokeza katika makala hii, ni makosa ya kiuchapaji hivyo hayahusiani na vyanzo rejelezi vilivyooneshwa hapo juu.
kazi nzuri
JibuFutakwa ujumla hii makala nimeipenda sana maana imeelezea vizuri sana
JibuFutanina swali pia,
toa maana ya tamthiliya ya majaribio na ujadili vipengele vyake.
shukrani kwa nakala yako nzuri
JibuFutamakala ya maana zaidi, heko.
JibuFuta