Ijumaa, 25 Machi 2016
DHANA YA UELEKEZI (TRANSITIVITY)
Dhana ya uelekezi imefafanuliwa na wataalamu mbalimbali kama ifuatavyo:
Vitenzi elekezi ni vitenzi ambavyo havijitoshelezi kisarufi vinahijia kutoshelezwa na yambwa moja au mbili ili vijikamilishe kisarufi (W.H.Whitely). Nomino inayokuja baada ya kitenzi inashikamana vipi na kitenzi husika. Ufafanuzi mpana wa dhana ya uelekezi unajikita katika namna mbalimbali za kukamilisha vitenzi.
Massamba (2004) anafafanua uelekezi kuwa ni uhusiano uliopo baina ya kitenzi na vijenzi vingine vya kimuundo wa sentensi vinavyohusiana nacho.
Habwe na Karanja (2004) wanaeleza kuwa uelekezi ni hali ya kitenzi kuruka mipaka na kuathiri maneno mengine ya sentensi. Maneno hayo yanayoathiriwa huwa ni yambwa au yambiwa.
Kihore (2001) anaona uelekezi kuwa ni uwezo wa kitenzi kinachoundwa na mzizi fulani kuchukuana na yambwa katika muundo wa sentensi.
Wren na Martin (2007) wanafasili kuwa uelekezi ni hali ya kitenzi kuashiria tendo linalofanywa na mtenda au kiima likiwa na yambwa.
Mkude (1995) anafafanua uelekezi kuwa ni uwezo wa kitenzi kujitosheleza kimuundo yaani iwapo kitenzi kinahitaji kujalizwa na kipashio kingine ili kifanye kazi kikamilifu.
Kwa ujumla, uelekezi ni dhana inayohusu hali ya kitenzi kubeba au kutobeba yambwa au yambiwa. Ni dhahiri kuwa dhana ya uelekezi ina uhusiano wa moja kwa moja na na kikundi tenzi. Hivyo ni vyema kukielewa vizuri kitenzi cha Kiswahili.
Kitenzi ni kategoria ambayo ni muhimili wa kikundi tenzi cha Kiswahili, ni nguzo au kielelezo muhimu cha sifa bainifu za lugha ya Kiswahili. Pamoja na kudokeza uelekezi, kitenzi cha Kiswahili hudokeza pia mambo mbalimbali kama vile kauli,njeo, hali nk.
AINA ZA VITENZI
Kwa kutumia kigezo cha uelekezi, wanasarufi wanagawa vitenzi vya Kiswahili katika makundi mawili nayo ni:
Vitenzi si elekezi
Vitenzi elekezi.
i.Vitenzi si elekezi
Hivi ni aina ya vitenzi ambavyo havihitaji kujalizwa na yambwa au yambiwa (kiathirika na mnufaikaji/ mfaidikaji) ili kukamilisha maana katika sentensi kama inavyooneshwa katika mifano ifuatayo:
Juma mto umejaa
Mbuzi amekufa
Ndege ameruka
Juma ameoa
Giza limeingia
Cesilia analia
Riziki anakoroma
Kikombe kimevunjika
Mvua zinanyesha
Easter amenuna nk.
Vitenzi katika sentensi hapo juu (a) hadi (f) hazihitaji yambwa kwa kuwa vitenzi vyenyewe vilivyotumika vinajitosheleza kimawasiliano (kimaana). Hatuwezi kwa mfano katika sentensi hizo tukabaki tunajiuliza maswali ambayo ni lazima yajibiwe. Mifano zaidi ya vitenzi hivyo ni duwaa, kua, zaa, ngaa, imba, kaa nk.
Vitenzi elekezi
Hivi ni vitenzi ambavyo huhitaji kujalizwa na nomino moja au mbili. Kwa maneno mengine, vitenzi elekezi ni vile vyenye uwezo wa kungoeka/ kubeba yambwa na/ au yambiwa. Vitenzi elekezi vyaweza kuwa elekezi kwa hulka yake au kwa kunyambuliwa. Unyambulishaji unaweza kuathiri kitenzi sielekezi kuwa elekezi kwa kukiongezea, kupunguza au kudhibiti vihusika vinavyoambatana nacho. Vitenzi elekezi vimegawanyika katika makundi mawili nayo ni:
Vitenzi elekezi mara moja
Vitenzi elekezi mara dufu
Vitenzi elekezi mara moja.
Hivi ni vitenzi elekezi vyenye kubeba yambwa moja tu. Chunguza mifano ifuatayo:
Shoo amejenga nyumba
Shembilu amenunua gari
Neema ameleta machungwa
Dada anapika ugali
Vitenzi vilivyomo katika sentesi hizo hapo juu zinahitajia yambwa moja ili kujikamilisha kimawasiliano. Mifano ya vitenzi vyenye hulka sawa na hivyo ni pamoja na beba, penda, iba, shusha, andika, chuma, soma nk. Vitenzi vyote hivyo vina tabia zinazofanana.
Vitenzi elekezi mara dufu
Hivi ni vile vitenzi ambavyo vinahitaji kujalizwa kwa yambwa mbili ili viweze kujikamilisha kisarufi. Mifano ifuatayo inadhihirisha ukweli huu:
Mwenyekiti amempa katibu ujumbe wake
Meneja alimkabidhi mhudumu mali zake
Jane alimpiga mpenzi wake kofi
Mwalimu alimpa mwanafunzi mimba
Vitenzi vyote katika sentensi hizo vinahitajia kufuatwa na yambwa zaidi ya moja. Vitenzi elekezi mara dufu siyo vingi sana katika lugha ya Kiswahili ukilinganisha na vitenzi elekezi mara moja.
DARAJIA ZA UELEKEZI
Uelekezi uko katika darajia mbili ambazo ni utendwa yaani kiathirika na utendewa yaani mfaidikaji/ mnufaikaji. Chunguza mifano ifuatayo:
Dada alimchumia baba yake maua
Mtoto alimuandikia baba barua
Mwajuma anampikia mmewe ugali
Nomino zilizokolezwa ni yambwa tendewa ambazo zinanufaika na tendo lenyewe na zile zisizokolezwa ni yambwa tendwa yaani zinzathirika na tendo moja kwa moja.
Ikiwa sentensi ina yambwa tendwa na tendewa, basi kitenzi chake hubeba kiambishi cha yambwa tendewa. Iwapo sentensi ina yambwa tendwa tu, basi kitenzi chake pia chaweza kubeba kiambishi yambwa. Kanuni hii inazua utata kuwa ni katika mazingira gani kiambishi yambwa chaweza kuwepo katika kitenzi na kutokuwepo katika kitenzi?? Chunguza mifano ifuatayo:
Kova anaikata nyama
Edo anamkatia nyama mama
Ali anamjengea baba nyumba
Fatuma alimnunulia shangazi gari
Mama anampikia mgeni ugali
Ukilinganisha mifano yote ya vitenzi vyenye uwezo wa kubeba yambwa utaona kuwa tofauti ya kungoeka au kutongoeka yambwa moja au mbili inathiri pia uwezo wa kitenzi kubeba au kutobeba kiambishi yambwa.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
mdau hujafafanua maana ya yambwa na yambiwa, naona umetaja tu
JibuFutaNashukuru sana,ila naomba unisaidie ni kwa vp uelekezi unaweza kuathiri vitenzi vya kiswahili
JibuFutaNzuri nimeelewa
JibuFutaNzuri nimeelewa
JibuFuta