Jumanne, 16 Juni 2015

DHANA YA KAMUSI NA MAUMBO NUKUZI YAKE



 Dhana ya kamusi imejadiliwa na wataalamu mbalimbali, na zimejibainisha kama ifuatavvyo;
TUKI ( 2004) wanaeleza, kamusi ni kitabu cha maneno yaliopangwa kwa utaratibu wa alfabeti na kutolewa maana kwa maelezo mengine.
Zgusta akinukuliwa na Mdee anaeleza, kamusi ni kitabu cha marerejeleo chenye msamiati ulio kusanywa kutoka kwa wazungumzaji wa jamii fulani na kupangwa katika utaratibu maalumu, kisha kufafanuliwa kwa namna ambayo wasomaji wanaweza kuelewa.
OXFORD  (2010)  wanaeleza kuwa kamusi ni kitabu ambacho kina orodha ya maneno ya lugha fulani katika mpangilio wa alfabeti na huelezwa maana ya maneno hayo. Pia  kamusi ni orodha ya maneno yaliopo katika mfumo wa kielektroniki mfano yanaweza kuhifadhiwa katika komputa.
Kwa ujumla kamusi ni kitabu kilichobeba orodha ya maneno mbalimbali ya lugha fulani yaliopangwa katika mpangilio wa kialfabeti na kutolewa maana zake kwa namna ambayo wasomaji wanaweza kuelewa.
Katika kueleza dhana ya maumbo nukuzi Abel  John, (2012) mwanafunzi wa chuo kikuu cha Dar Es Slaam katika makala ya Kiswahili anaeleza kuwa maumbo nukuzi  ni umbo la msingi la neno, mfano;  maneno lima, cheza, kula, imba na soma.
 Kwa ujumla, maumbo nukuzi ni umbo la msingi la neno linaloingizwa katika kamusi na kusimama kama kidahizo katika kamusi, hivyo maneno kama vile imba, lima na cheza ni maumbo msingi ya maneno yaingizwayo katika kamusi, mathalani husimama katika vidahizo.
Maumbo nukuzi yapatikanayo katika kamusi ni kama vile:
Maumbo sahili, Haya ni maneno huru yasiyo na utegemezi  au yasiyo na utegemezi, mfano; baba, mama, barua, bakuli, nyumba na cheza, haya ni maumbo huru yasiyo na utegemezi na huingizwa katika kamusi kama vidahizo.
Maumbo ambatani, Haya ni maneno ambayo huumbwa kwa kuunganishwa maneno mawili tofauti kama vile nomino na kitenzi, nomino na nomino na maneno mengine. Katika  kamusi maneno haya huchukuliwa kama neno moja lenye kuwakilisha dhana fulani. Maumbo haya yamejitokeza katika kamusi ya TUKI [2001] kama vile:
                    Kipaza+sauti                 kipazasauti
                   Kipasha+moto                kipashamoto
                   Kipima+hewa                 kimahewa
Maneno haya yote ni mwambatano lakini husimama kama neno moja katika kamusi na katika kamusi hatuangalii neno moja moja bali hata misemo na nahau ambayo pia huchukuliwa kama neno moja lenye kuwakilisha dhana fulani. Mfano  TUKI(2001) wametoa mifano kama vile:
                Kifungua +kinywa                    kifunguakinywa
               Tia+nanga                                 tiananga
               Piga+maji                                  pigamaji
Licha ya maneno haya kuwa yana uambatani wa zaidi ya neno moja, hutoa maana moja yenye kueleza dhana fulani inayobebwa na maneno haya.
Maumbo hulutishi, haya ni maumbo ya maneno ambayo hutokea kama kidahizo katika kamusi, maneno haya huuundwa kwa kuunganisha sehemu mbili za maneno tofauti na sio sehemu nzima. Oxford (2010)  wametoa mifano kama vile:
Telephone
Mobitel                               mobile telephone
Telefax
Maneno haya ni sehemu ya maneno fulani ambayo husimama kama kidahizo na kutoa maana iwakilishwayo na maneno hayo yaliyo hulutishwa.
Maumbo ya Akronimia, haya ni maumbo ambayo huingizwa katika kamusi kama kidahizo na huwa na ufupisho ambao huwakilishwa kwa herufi kubwa ambapo kila herufi hubeba maana fulani. Kamusi  ya Oxford (2006) imetoa mifano kama vile:
           ISBN                                     International Standard Book Number.
           ISDN                                   International Granted service Digital Network.
Akronimia hizi hutokea upande wa kidahizo kuwakilisha maana au dhana iliyo ndefu kuwa katika maneno machache.
Maumbo rejezi, Haya ni maumbo ya kumfanya msomaji arejee ili kupata ufafanuzi zaidi. Katika  kamusi huoneshwa kwa kutumia alama ya mshale ambao hulenga kumuonesha msomaji kulitafuta neno linalooneshwa ambalo lina uhusiano na kidahizo kinachoshughulikiwa na msomaji, iliawze kupata uelewa wa kina juu ya kidahizo hicho.
Mfano TUKI (2010) Wameonesha urejezi kama vile
               Pas.try                      see also
               pipe                           see also pin pipes
Mshale huu huwekwa baada ya taarifa ya kidahizo husika ili kumfanya msomaji aweze kurejea kidahizo fananifu na kinafanana na kile kinachoshughulikiwa na msomaji.
Maumbo dondoshi, Ni maumbo ambayo huingizwa katika kamusi kama kidahizo baada ya sehemu ya neno hilo kudondoshwa. Mfano Oxford (2010) wametoa mifano kama vile:
               Phone from telephone
              Gram from telegram
             Bike from bicycle.
Maumbo haya hubeba maaana ambayo hupatikana katika neno zima kabla hata halijafupishwa.
Maumbo radidi, Ni maumbo ya neno linalojirudia katika kamusi na neno hilo hubeba dhana moja katika kamusi.
       Mifano: -   urambembe
       -   Myungiyungi

Maumbo haya hubeba dhana moja inayowakilishwa na uradidi huo.
Maumbo ya homonimia, Ni maumbo ambayo huwa sawa katika maandishi, matamshi lakini huwa tofauti katika maana za maneno hayo, katika kamusi maneno haya hutofautishwa  kwa kupewa namba, mfano,
Kaa1
Kaa2
Kaa3
Na tofauti ya maneno  haya yanaonekana katika kitomeo, yaani maelezo yatakayotolewa kuhusiana na kidahizo hicho.
 Kando na maumbo nukuzi, kamusi pia ina matatizo yake, nayo ni kama yafuatayo;
Upotezaji wa uasili wa asili ya kidahizo husika. Katika  uandaaji wa kamusi kuna baadhi ya maneno hupoteza uasili wake pindi yanapoandikwa na kuingizwa kama vidahizo. Mfano maneno kama;
                    Kusoma                                   soma
                   Kuimba                                     imba
                   Kucheza                                    cheza
Kutokana na tatizo hili inashauriwa kuingiza vidahizo katika myambuliko na kuweka utangulizi unaoeleza kuwa umeingiza vitenzi kutokana na mzizi. Mfano,
                   Kucheza, chezea, chezesha na  chezeka yameingizwa kutokana na mzizi ‘ chez’
                  ambayo husimama kama kidahizo ‘cheza’.
Tatizo lingine ni utofauti wa matamshi wa lahaja moja ambayo huwa vigumu kuweka vibadala vyote. Mfano,
                  Bomba la maji- watu wa bara huita bomba
                                          -watu wa pwani huita kifereji
Hii hupelekea mtunzi wa kamusi kupata shida katika kufafanua dhana hii kwa kuwa na lahaja zaidi ya moja. Kutokana na tatizo hili inashauriwa kuchagua vidahizo katika lahaja moja na kuweka utangulizi  unaotolea ufafanuzi juu ya lahaja iliyoandikiwa sana.
 Tatizo la mwisho ni kupanga vidahizo kialfabeti. Hili pia ni tatizo kwani wanalugha wanafahamu  maneno ya lugha kiasili yake, hawafahamu isimu na maneno magumu kupanga kialfabeti. Mfano ,
                          Kucheza  kuwa cheza 
                          Kupika  kuwa  pika
Maneno yote haya hutafutwa katika kamusi kwa kufuata mpangilio wa kialphabeti. Hii husababisha wanalugha kushindwa kutafuta maneno  wanayohitaji kupata dhana zake. Kutokana na tatizo hili inashauriwa kuweka utangulizi mzuri utakaoonesha mpangilio wa alfabeti  zilizotumika katika uwekaji wa vidahizo hivyo ili iwe rahisi kwa mwanalugha yeyote kutafuta dhana ya neno aliolikusudia kwa haraka. Mfano,   Kamusi ya Kiswahili ya F. Johnson (1962-vi ) anatolea maelezo juu ya utangulizi wake kama ifuatavyo;
                       Maneno yamepangwa kufuata taratibu ya alfabeti, yaani a, b, ch, d, e, f, g, h, I, j,
                      k, l, m, n,  o, p, r, s, t, u, v, w, y, z.
Pia anaendelea kutoa ufafanuzi katika (viii) anasema,
                    kwa ajili ya watu wasiojua Kiswahili sana, tumeonyesha namna ya kufanya maneno
                   ya wingi ya majina hivi. Kitabu, vi-; pipa, ma-; mtu, wa-; ulimi (ndimi); nk; yaani
                  neno la wingi la kitabu ni vitabu, la pipa ni mapipa, la mtu ni watu, la ulimi ni ndimi.
                 Majina yote yamepigwa chapa kuanzia herufi kubwa.
Kwa ujumla kumusi husaidia kwa kiasi kikubwa kukuza lugha kutokana na wanalugha kupata dhana  za maneno mbalimbali kutoka kwenye kamusi na kuyatumia. Hii husaidia misamiti mbalimbali kutumika kwa kiasi kikubwa na kuenea ua kusambaa kwa wanalugha wengi, ambayo hupelekea kukua na kuenea kwa lugha kwa ujumla.


MAREJELEO.
F. Johnson (1962), Kamusi ya Kiswahili. The Sheldon Press: London.
Oxford (2010), Oxford Advanced Learners  Dictionary. Oxford  University Press: New York.
TUKI (2004), Kamusi  ya Kiswahili Sanifu. TUKI: Dar es esaalam.
                                

 TANBIHI: Kwa makosa ya kitahajia na kimaana yanayoweza kujitokeza kwenye kazi hii nia makosa  ya kiuchapaji hayahusiani na vyanzo rejewa vilivyotumika.                            



                      



 



 



 






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni