Ijumaa, 20 Mei 2016

                       MCHANGO WA FASIHI KWA WABANTU

Neno Bantu maana yake ni watu katika lugha nyingi za kundi hilo. Mtaalam Wilhelm Heinrich Immanuel Bleek aliyeishi tangu mwaka 1827-1875, alitumia neno hilo kwa kurejelea kundi la lugha za kibantu. Aliendelea kusema kuwa wabantu wenyewe ni wakulima na wafugaji waliotokea maeneo ya kaskazini mwa Kameruni na kuja hadi katika upwa wa Afrika Mashariki na maeneo mengine. Sababu zilizopelekea Wabantu kuhama kutoka katika maeneo yao ya asili na kuhamia sehemu nyingine ni kutokana na vita, ukame, njaa pamoja na magonjwa yaliyowakumba katika jamii zao. Wabantu si washenzi kwani walikuwa na mifumo yao ya uongozi na mifumo mingine ya kimaisha kama jamii nyingine. Jamii za wabantu zaidi ya makundi mia nne (400) yalienea barani Afrika na kueneza lugha zao za kibantu kwani ndizo zilizokuwa zikitumika katika mawasiliano. Mfano nchi kama Nigeria, Kameruni, Guinea ya Ikweta, Gabon, Jamuhuri ya Kongo, Rwanda, Burundi, Uganda, Kenya na Tanzania jamii zake nyingi zinatumia lugha za kibantu katika mawasiliano.
Bantustani ni ardhi waliyotengewa Waafrika weusi wa nchi ya Afrika Kusini wakati wa kipindi cha ubaguzi wa rangi, wakati ambapo jamii za Afrika Kusini zilivyochangamana na jamii nyingine za kigeni kutoka Ulaya na Asia.
Negro ni neno lililokuwa likitumika na watumiaji wa lugha ya kiingereza kumaanisha mtu mweusi, hivyo basi M-Negro ni mtu mweusi. Kwa ujumla M-bantu na M-negro wote ni watu weusi wenye asili ya Afrika.
Ushenzi ni hali ya kuwa nyuma kimaendeleo na kutenda matendo ya kijinga na kikatili au ni hali ya kutostarabika (Kamusi ya Kiswahili Sanifu).Kwa mujibu wa maana hii ya ushenzi, si kweli kuwa wabantu ni mishenzi yaani ni watu wasiostaarabika na walio nyuma kimaendeleo. Wabantu kihistoria inathibitika kuwa na mifumo yao ya kimaisha, shughuli zao za uzalishaji mali kama vile kilimo, ufugaji na shughuli nyingine za kijamii. Pia wabantu walikuwa na tamaduni zao, mila na desturi zinazothibitisha kuwa wabantu hawakuwa washenzi.
Dhana ya fasihi imefasiliwa na wataalam mbalimbali wa fasihi kwa mitindo na miono yao tofauti, baadhi ya wataalam hao ni kama vile;
Fasihi ni Sanaa yaani mkusanyiko wa kazi mbalimbali zilizosanifiwa kwa kutumia lugha itumiayo Zaidi maneno na kujishughulisha na jinsi binadamu anavyojitambua mwenyewe binafsi, pia  anavyoathiriwa na binadamu wenzake  aidha na vingine aina kwa aina katika mazingira mbalimbali  ya maisha (Nkwera, F.V,(2003:94).
Fasihi ni sanaa itoayo maudhui yake kwa kutumia lugha ya maneno ambayo hutamkwa ama kuandikwa (Senkoro F.E, 2011:11).
Fasihi ni Sanaa ya lugha inayoshughulikia masuala yanayohusu binadamu matatizo yake, ndoto zake, matumaini yake, migogoro yake, na jinsi anavyoingiliana na mazingira yake (Wamitila, 2004:19)
Kwa ujumla, fasihi ni sanaa itumiayo lugha  katika ustadi wa  hali ya juu na wenye kueleweka  katika kufikisha ujumbe kwa  hadhira au jamii lengwa, kuburudisha, kuonya, kukejeri, na hata kukashifu kwa njia ya maandishi au masimulizi. Fasihi kama sanaa itumiayo maneno, inajenga picha halisi ya mwanadamu katika maisha yake, mahusiano yake na viumbe wengine, migogoro yake na mazingira, shida zake, raha zake, matumaini yake na jinsi anavyopiga hatua katika maendeleo yake.  Fasihi bila kujali ni fasihi andishi au fasihi simulizi imekuwa na mchango mkubwa kwa jamii ya watu mbalimbali na kusaidia jamii hizo au watu hao wasiendelee kujitukana na kujiita M-BANTU na M-NEGRO kama ifuatavyo;
Fasihi imesaidia kuchochea uzalishaji mali katika jamii; kutokana na shughuli au kazi mbalimbali za fasihi, fasihi imesaidia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za uzalishaji mali. Tangu enzi za ujima fasihi ilitumika Kama nyenzo mojawapo ya uzalishaji Mali. Jamii zilipata kutumia nyimbo Kama nyenzo mojawapo ya uzalishaji Mali katika shughuli za kilimo, uwindaji na shughuli nyingine za kijamii. Kwa kuwa fasihi inabadilika kulingana na mazingira na wakati, fasihi imetoa mchango mkubwa hadi leo katika shughuli za uzalishaji mali. Kuna nyimbo mbalimbali zinazohamasisha kazi. Kwa mfano wimbo wa Vijana fungeni mikanda wa TMK Wanaume Family na wimbo wa Vicky Kamata Wanawake na Maendeleo ni baadhi tu ya nyimbo nyingi zinazo hamasisha kazi katika jamii.Vile vile methali kama vile Asiyefanya kazi na asile, Mga gaa na upwa hali wali mkavu, haba na haba hujaza kibaba, ndo ndo ndo si chululu ni mifano ya kazi za fasihi zinasaidia kuhamasisha shughuli za uzalishaji mali katika jamii za wabantu. Pia katika  fasihi andishi, kuna vitabu kama vile Kijiji ChetuWasifu wa Siti Binti Saadi, Nguzo Mama, ni miongoni mwa kazi za fasihi andishi zinazochochea uzalishaji mali kwa jamii za wabantu. Kwa mifano ya kazi hizo na nyingine nyingi za kifasihi, ni dhahiri shahiri kuwa fasihi imetusaidia tusiendee kujitukana kwa kuchochea maendeleo na kujenga jamii yenye misingi ya kujitegemea katika nyanja mbalimbali za kimaisha.Misingi hiyo katika jamii za kibantu zinajitokeza katika ngazi ya familia hadi ngazi ya taifa hususani katika nchi yetu, kwani hadi sasa sera inayotawala bado inachochea shughuli za uzalishaji mali na kufanya kazi (Hapa kazi tu,)
Fasihi imesaidia katika ujenzi wa jamii mpya zenye macho na fikra pambanuzi.Fasihi imesaidia kuibua fikra za kimapinduzi zinazosaidia jamii kuhama katika hali moja hadi nyingine. Uwepo wa kazi mbalimbali za kifasihi umesaidia kuibua fikra za mapinduzin zinazopinga masuala ya uongozi mbaya, rushwa, uhujumu uchumi na ukasuku kwa viongozi. Pia kupingaa fikra kandamizi na za kibaguzi katika jamii. Kwa mfano, nyimbo kama vile Mjomba ya Mrisho Mpoto, Keki ya Taifa ya Wakoloni na Songa, Kikao cha dharura ya profesa Jay,  ni nyimbo zinazopambanua maovu katika  mfumo wa serikali, na kujaribu kutoa ushauri juu ya nini kifanyike ili kusawazisha mfumo wa kiutawala kwa kufuata sera ya utawala bora. Pia katika fasihi andishi, kuna vitabu mbalimbali vya riwaya, tamthiliya na ushairi vinavyopinga masuala mbalimbali kama vile uongozi mbaya, rushwa, uhujumu uchumi na mengine mengi yanayokwamisha na kurudisha nyuma maendeleo ya jamii. Kwa mfano vitabu kama vile Msomi Aliyebinafsishwa, Wasakatonge, Mabepari wa Bongo, Kivuli Kinaishi na vingine vingi ni baadhi tu ya kazi nyingi za fasihi andishi zinasawiri mifumo mibovu ya serikali, rushwa, uhujumu uchumi katika jamii mbalimbali. Hivyo basi kutokana na kazi hizo fasihi imetusaidia kutoendelea kujitukana wenyewe kwa kuwa na mifumo mibovu ya kiuongozi na utawala kwa ujumla. Fasihi imetuasa kuachana na mambo hayo yanayokwamisha maendeleo na kuamua kujenga jamii mpya yenye itikadi na mambo yanayonufaisha jamii kwa ujumla na wala si watu wachache, kwani tangu awali wabantu na wanegro walikuwa na mifumo bora ya kiutawala isiyobagua wala kunyanyasa watu wake.
Fasihi imesaidia kuachana na mila na desturi zilizopitwa na wakati na zenye madhara katika jamii. Kutokana na kazi mbalimbali za kifasihi, jamii imeachana na mila na desturi kandamizi na za kibaguzi katika jamii. Kwa mfano fasihi imesaidia kupiga vita watoto wa kike kuchaguliwa wanaume wa kuwaoa. Fasihi imesaidia kupiga marufuku suala hilo na kwa namna moja ama nyingine imeonesha njia ya mafanikio.Kuna nahau kama vie mapenzi majani huota popote, penzi kikohozi kulificha huwezi, asiyekupenda hakuthamini, ni baadhi tu ya amali za fasihi simulizi zinapinga hali ya wazazi kuchagulia watoto wao wake au waume wa kuishi nao kuwa ni makosa. Kila mtu ana moyo na moyo huwa na chaguo lake hivyo ni vyema moyo ukachagua kile kitakacho furahisha moyo na wala si kuchaguliwa Mfano katika kitabu cha Vuta N′kuvute Yasmini anapochaguliwa mume wa kuishi nae na wazazi wake ambaye hakumridhia kunasasbabisha ndoa hiyo kuvunjika.Pia kuachana na mauaji ya albino, fasihi  kwa kupitia nyimbo na tanzu nyingine inapinga vikali mauaji ya albino au watu kuuana wenyewe kwa wenyewe kwa minajiri ya kupata pesa na kuwa matajiri. Fasihi inaionya jamii juu ya suala hilo kwani albino anaweza kuishi na kufanya kazi kama binadamu wengine.Mfano nyimbo ya Kilimanjaro music Tusiue albino, misemo kilema nae mtu, usimcheke chongo ni baadhi ya kazi za fasihi zinazopinga watu kubaguana katika jamii kwa sababu za kimaumbile, rangi, nasaba zao kwa namna moja ama nyingine. Katika fasihi andishi hali hii ya kupinga mauji ya albino na ubaguzi kwa ujumla inajidhihirisha katika kitabu cha Takadini. Hivyo basi tunaona namna ambavyo fasihi ilivyoweza kutusaidia kupinga tamaduni zilizopitwa na wakati kama vile kuua albino, kuchaguliwa mume au mke wa kuoa, kutowasomesha atoto wa kike na mengine mengi yanayotufanya tusiendelee kujitukana wenyewe kwa kuwa Wabantu au Wanegro.
Kulinda maslahi ya taifa, fasihi imeonesha mambo ambayo yanalenga kulinufaisha taifa bila kujali rangi wala kabila kwa manufaa ya jamii nzima. Fasihi imeweza kukemea matendo maovu yanayofanywa na baadhi ya viongozi kwa manufaa yao binafsi na kufanya taifa kuwa katika hali ya umaskini. Mfano katika kitabu cha Msomi Aliyebinafsishwa mwandishi anaonesha matatizo ya wasomi kupenda kujinufaisha wenyewe kwa kujilimikizia mali bila kujali taifa. Pia mambo ya uongozi mbaya ambao haulengi kuwanyonya watu wa hali ya chini. Mfano katika kitabu cha Kisiwa cha Giningi.
Vilevile katika fasihi simulizi, masimulizi mbalimbali ya zamani yaliyokuwa yanasimuliwa kwa lengo la kufanya watu kulinda na kupenda utaifa kuliko watu binafsi, nyimbo na matambiko ya kale yalilenga kujenga mshikamano na kulinga maslahi yao kama jamii moja.Mfano misemo kama vile, nyumbani ni nyumbani, mkataa kwao ni mtuwa ni amali za fasihi simulizi zinazohamasihsa kuthamini na kulinda maslahi ya taifa kwa ujumla bila kuangalia mtu mmoja mmoja. Hii ni ishara kubwa kwamba fasihi imetusaidia tusiendelee kujitukane wenyewe kwa kujiita Mbantu,Mnegro badala yake kulinda taifa zima dhidi ya madhira ya dunia kama vile magonjwa kama vile UKIMWI, EBOLA, mafuriko na mengine mengi.
Fasihi imesaidia kueneza itikadi mbalimali, fasihi kama sanaa imeweza kueneza itikadi husika kwa kipindi tofauti tofauti. Mfano katika kipindi cha ukoloni fasihi ilioweza kupinga ukoloni kwa mfano, methali kama vile Mzungu katupwa jalalani, misemo kama vile kupe, mabeberu.  Amali zote hizo za fasisihi simulizi zilikuwa na malengo ya kumnyanyapaa mkoloni kwani ni mtu asiye na huruma kwa waafrika.Pia nyimbo mbalimbali zilitungwa kupiga vita ukoloni kutokana na mabaya yote.
Katika fasihi andishi itikadi za wabantu na wanegro kwa ujumla bado zimejitokeza kwa namna moja ama nyingine ikiwa ni kupinga itikadi za kikoloni. Mfano katika vitabu kama vile Mashairi ya Saadan Kandoro, Ubeberu Utakwisha, kinjekitile na vingine vingi vilivyoandikwa kwa lengo la kupinga itikadi na mifumo ya kikoloni ambayo iliharibu mifumo ya awali ya wabantu. Hivyo basi, fasihi imetusaidia kuendeleza itikadi zetu za awali na kufanya tusijitukane wenyewe kwani kutetea mifumo yetu ya awli ni dhahiri kuwa haikuwa na chembe yoyote ya kibaguzi wala unyanyasaji kiutawala na kijamii.
Kuhifadhi amali za jamii;fasihi ni kama ghala la kuhifadhia amali mbalimbali za jamii yaani tamaduni pamoja na historia ya jamii huika.Katika kuhifadhi amali za jamii fasihi inakuwa nyenzo muhimu.Aidha wanajamii hufahamishwa kifasihi historia yao,wao ni nani na wanachimbukia  wapi.Maarifa haya ni muhimu kwa wanajamii hususani wabantu kwani husaidia sio tu kujielewa bali pia kujitambua.Zipo kazi mbalimbali ambazo zinaelezea historia ya wabantu kama vile Moto wa mianzi ambayo huelezea historia ya wahehe,Zawadi  ya ushindi amabayo huelezea vita ya kagera na Kinjekitile.Kuepo kwa kazi hizo za fasihi inaonesha kuwa wabantu wana historia yao na si  washenzi bali nao wana  maendeleo ambayo yamefikiwa.Fasihi imesaidia kwa kiasi kikubwa wabantu wasiendelee kujitukana kwa kuwa fasihi inaeleza historia yao vilevile kutunza amali za jamii mbalimbali za wabantu.Amali za jamii kama vile ngoma,nyimbo,ngonjera,ngomezi na semi mbalimbali hutunzwa na fasihi katika jamii za wabantu.
Kukuza na kueneza stadi za lugha za wabantu.kwa kuwa fasihi hutegemea sana katika lugha hivyo basi semi, hadithi, vitendawili na kuimba hutumia lugha ambazo miongoni mwazo hutumiwa na wabantu.Fasihi simulizi kwa mfano ina mchango mkubwa miongoni mwa wabantu katika kuzimiliki stadi za lugha zao.Kutumika kwa lugha za wabantu katika fasihi inaonesha kuwa wabantu wana lugha zao na wala si washenzi (watu wasio na maendeleo).kiswahili kama lugha ya wabantu kimekuwa na kuenea kutokana na fasihi.
Kuunganisha jamii au vizazi;fasihi imesaidia katika kuunganisha  kizazi kimoja hadi kingine katika vipindi mbalimbali.Kwa mfano hapo awali ushairi wa Kiswahili ulikuwa ukitungwa kimasimulizi na baadae ukaanza kutungwa kimaandishi miongoni mwa jamii za watu  katika upwa wa Afrika mashariki.Maendeleo ya fasihi kutoka katika fasihi simulizi hadi katika fasihi andishi kumeunganisha  vizazi vya kale vya wabantu na vilivyopo na vijavyo.Kutokana na kukuwa kwa Kiswahili kazi mbalimbali za fasihi kama vile ushairi,tamthiliya na riwaya zilitungwa kwa kuzingatia utamaduni wa jamii pana.Fasihi ni msingi wa kuunganishia  wanajamii(wabantu)waliopo na waliopita kwa kutambiwa hadithi,methali na nyimbo zao.
Kuongeza pato miongoni mwa wabantu;Kazi mbalimbali za fasihi zina umuhimu kwa wabantu kwa sababu husaidia  wasiendelee kujitukana kuwa wao ni washenzi hii ni kutokana  na fasihi huweza kuwasukuma mbele wabantu katika hali ya chini ya kimaisha mpaka katika hali nzuri ya maisha.Kwa mfano katika majigambo,methali,mashairi hadithi,vitendawili,nahau,riwaya na tamthiliya ni kazi za kifasihi zinanozo saidia ili wabantu wasiendelee kujitukana kama wao ni washenzi.kwa mfano kuna nahau na misemo mbalimbali ambazo ni kichocheo cha maendeleo katika jamii za wabantu.Kwa mfano “Misitu ni mali” na “maji ni uhai”.Methali kama vile “haba na haba hujaza kibaba”,”Mtegemea cha ndugu hufa masikini”,”Ukitaka cha mvunguni sharti uiname”,vilevile kuna kazi kama za majigambo ambazo huonesha ushujaa katika mambo mbalimbali.kwa mfano wa  majigambo;
                                                    “Mimi ni,
                                                      Mahali-pa-juu.azaae matunda,
                                                      Kamba ya kupandia ifikishayo kwenye kilele
                                                      Cha mnazi (yaani cheo cha ‘eze’)
                                                       Kisu kivunacho pesa
                                                        Utajiri kutoka juu
                                                       Mgombanaji awagombaniaye nduguze
                                                        Mkulima alimaye njaa (Ili kuikomesha).
Majigambo kama hayo huhamasisha wabanyu katika harakati za kujikwamua kimaisha miongoni mwao.
Vilevile kazi za fasihi andishi husaidia katika kuongeza pato. Kwa mfano kuuza vitabu kama vile vya riwaya,ushairi na tamthiliya husaidia kuongeza pato na kusaidia kuwaendeleza wabantu katika hali ya kiuchumi.Kuendelea kiuchumi miongoni mwa wabantu kumesaidia wasiendelee kujitukana kuwa wao ni washenzi bali ni watu wenye maendeleo yao kama zilivyo jamii nyingine.
Kwa ujumla, fasihi imetusaidia tusiendelee kujitukana kutokana na ukweli kuwa fasihi inadhima nyingi katika maisha ya kila siku ya binadamu japokuwa huwa inabadilika kulingana na mazingira na wakati. Fasihi imesaidia kuainisha vipengele anuai vya kimaisha vinavyotakiwa kuendelezwa na kuachwa kama vile mauaji ya albino na tamaduni za kale zilizopitwa na wakati. Fasihi pia imetusaidia kuonya na kuadabisha jamii vile vile kuelimisha jamii, kwa mfano kuelimisha jamii juuu ya masuala ya UKIMWI kupitia nyimbo mfano wimbo wa Feruzi ‘starehe’, masimulizi, nahau na hata misemo mbalimbali ili kujikinga na gonjwa hilo la hatari.

                                               Marejeleo.
Amatu.J.K ,(2003),Fasihi Simulizi.Mvule Africa Publsher:Nairobi
Kabuta.N.S ,(1197),Isimu-Ushairi:Muundo wa majigambo.University of Genk:Genk
Maitaria.J.N,(2003),Methali kama formula katika utunzi wa uwasilishaji wa ushairi wa Kiswahili.Chuo kikuu cha Kenyatta:Nairobi.
Msuya A.B (2008).Semi, Maana na Matumizi. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo kikuu cha Dar es salaam.
Sengo T.S (1992) Tungo za Pwani.Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Senkoro F. E (2011).Fasihi. Kautu Limited. Dar es Salaam.
TUKI,(2005),Kamusi ya Kiswahili.Oxford university press:Dar es salaam.
Wamitila K.W (2004).Kichocheo cha Fasihi Siulizi na Andishi. Focus Publishers ltd. Nairobi.

 TANBIHI; Makosa ya kiothografia yatakayojitokeza katika makala hii ni makosa ya kiuchapishaji na siyo ya vyanzo vilivyorejelewa.

Ijumaa, 25 Machi 2016



                     DHANA YA UELEKEZI (TRANSITIVITY)
Dhana ya uelekezi imefafanuliwa na wataalamu mbalimbali kama ifuatavyo:
Vitenzi elekezi ni vitenzi ambavyo havijitoshelezi kisarufi vinahijia kutoshelezwa na yambwa moja au mbili ili vijikamilishe kisarufi (W.H.Whitely). Nomino inayokuja baada ya kitenzi inashikamana vipi na kitenzi husika. Ufafanuzi mpana wa dhana ya uelekezi unajikita katika namna mbalimbali za kukamilisha vitenzi.
Massamba (2004) anafafanua uelekezi kuwa ni uhusiano uliopo baina ya kitenzi na vijenzi vingine vya kimuundo wa sentensi vinavyohusiana nacho.
Habwe na Karanja (2004) wanaeleza kuwa uelekezi ni hali ya kitenzi kuruka mipaka na kuathiri maneno mengine ya sentensi. Maneno hayo yanayoathiriwa huwa ni yambwa au yambiwa.
Kihore (2001) anaona uelekezi kuwa ni uwezo wa kitenzi kinachoundwa na mzizi fulani kuchukuana na yambwa katika muundo wa sentensi.
Wren na Martin (2007) wanafasili kuwa uelekezi ni hali ya kitenzi kuashiria tendo linalofanywa na mtenda au kiima likiwa na yambwa.
Mkude (1995) anafafanua uelekezi kuwa ni uwezo wa kitenzi kujitosheleza kimuundo yaani iwapo kitenzi kinahitaji kujalizwa na kipashio kingine ili kifanye kazi kikamilifu.
Kwa ujumla, uelekezi ni dhana inayohusu hali ya kitenzi kubeba au kutobeba yambwa au yambiwa. Ni dhahiri kuwa dhana ya uelekezi ina uhusiano wa moja kwa moja na na kikundi tenzi. Hivyo ni vyema kukielewa vizuri kitenzi cha Kiswahili.
Kitenzi ni kategoria ambayo ni muhimili wa kikundi tenzi cha Kiswahili, ni nguzo au kielelezo muhimu cha sifa bainifu za lugha ya Kiswahili. Pamoja na kudokeza uelekezi, kitenzi cha Kiswahili hudokeza pia mambo mbalimbali kama vile kauli,njeo, hali nk.

AINA ZA VITENZI
Kwa kutumia kigezo cha uelekezi, wanasarufi wanagawa vitenzi vya Kiswahili katika makundi mawili nayo ni:
Vitenzi si elekezi
Vitenzi elekezi.

i.Vitenzi si elekezi
Hivi ni aina ya vitenzi ambavyo havihitaji kujalizwa na yambwa au yambiwa (kiathirika na mnufaikaji/ mfaidikaji) ili kukamilisha maana katika sentensi kama inavyooneshwa katika mifano ifuatayo:
Juma mto umejaa
Mbuzi amekufa
Ndege ameruka
Juma ameoa
Giza limeingia
Cesilia analia
Riziki anakoroma
Kikombe kimevunjika
Mvua zinanyesha
Easter amenuna nk.

Vitenzi katika sentensi hapo juu (a) hadi (f) hazihitaji yambwa kwa kuwa vitenzi vyenyewe vilivyotumika vinajitosheleza kimawasiliano (kimaana). Hatuwezi kwa mfano katika sentensi hizo tukabaki tunajiuliza maswali ambayo ni lazima yajibiwe. Mifano zaidi ya vitenzi hivyo ni duwaa, kua, zaa, ngaa, imba, kaa nk.

Vitenzi elekezi
Hivi ni vitenzi ambavyo huhitaji kujalizwa na nomino moja au mbili. Kwa maneno mengine, vitenzi elekezi ni vile vyenye uwezo wa kungoeka/ kubeba yambwa na/ au yambiwa. Vitenzi elekezi vyaweza kuwa elekezi kwa hulka yake au kwa kunyambuliwa. Unyambulishaji unaweza kuathiri kitenzi sielekezi kuwa elekezi kwa kukiongezea, kupunguza au kudhibiti vihusika vinavyoambatana nacho. Vitenzi elekezi vimegawanyika katika makundi mawili nayo ni:

Vitenzi elekezi mara moja
Vitenzi elekezi mara dufu
         
Vitenzi elekezi mara moja.
Hivi ni vitenzi elekezi vyenye kubeba yambwa moja tu. Chunguza mifano ifuatayo:
Shoo amejenga nyumba
Shembilu amenunua gari
Neema ameleta machungwa
Dada anapika ugali

Vitenzi vilivyomo katika sentesi hizo hapo juu zinahitajia yambwa moja ili kujikamilisha kimawasiliano. Mifano ya vitenzi vyenye hulka sawa na hivyo ni pamoja na beba, penda, iba, shusha, andika, chuma, soma nk. Vitenzi vyote hivyo vina tabia zinazofanana.

Vitenzi elekezi mara dufu
Hivi ni vile vitenzi ambavyo vinahitaji kujalizwa kwa yambwa mbili ili viweze kujikamilisha kisarufi. Mifano ifuatayo inadhihirisha ukweli huu:

Mwenyekiti amempa katibu ujumbe wake
Meneja alimkabidhi mhudumu mali zake
Jane alimpiga mpenzi wake kofi
Mwalimu alimpa mwanafunzi mimba

Vitenzi vyote katika sentensi hizo vinahitajia kufuatwa na yambwa zaidi ya moja. Vitenzi elekezi mara dufu siyo vingi sana katika lugha ya Kiswahili ukilinganisha na vitenzi elekezi mara moja.

                       DARAJIA ZA UELEKEZI
Uelekezi uko katika darajia mbili ambazo ni utendwa yaani kiathirika na utendewa yaani mfaidikaji/ mnufaikaji. Chunguza mifano ifuatayo:

Dada alimchumia baba yake maua
Mtoto alimuandikia baba barua
Mwajuma anampikia mmewe ugali

Nomino zilizokolezwa ni yambwa tendewa ambazo zinanufaika na tendo lenyewe na zile zisizokolezwa ni yambwa tendwa yaani zinzathirika na tendo moja kwa moja.

Ikiwa sentensi ina yambwa tendwa na tendewa, basi kitenzi chake hubeba kiambishi cha yambwa tendewa. Iwapo sentensi ina yambwa tendwa tu, basi kitenzi chake pia chaweza kubeba kiambishi yambwa. Kanuni hii inazua utata kuwa ni katika mazingira gani kiambishi yambwa chaweza kuwepo katika kitenzi na kutokuwepo katika kitenzi?? Chunguza mifano ifuatayo:

Kova anaikata nyama
Edo anamkatia nyama mama
Ali anamjengea baba nyumba
Fatuma alimnunulia shangazi gari
Mama anampikia mgeni ugali

Ukilinganisha mifano yote ya vitenzi vyenye uwezo wa kubeba yambwa utaona kuwa tofauti ya kungoeka au kutongoeka yambwa moja au mbili inathiri pia uwezo wa kitenzi kubeba au kutobeba kiambishi yambwa.