Neno Bantu maana yake ni watu katika lugha
nyingi za kundi hilo. Mtaalam Wilhelm Heinrich Immanuel Bleek aliyeishi tangu
mwaka 1827-1875, alitumia neno hilo kwa kurejelea kundi la lugha za kibantu.
Aliendelea kusema kuwa wabantu wenyewe ni wakulima na wafugaji waliotokea
maeneo ya kaskazini mwa Kameruni na kuja hadi katika upwa wa Afrika Mashariki
na maeneo mengine. Sababu zilizopelekea Wabantu kuhama kutoka katika maeneo yao
ya asili na kuhamia sehemu nyingine ni kutokana na vita, ukame, njaa pamoja na
magonjwa yaliyowakumba katika jamii zao. Wabantu si washenzi kwani walikuwa na
mifumo yao ya uongozi na mifumo mingine ya kimaisha kama jamii nyingine. Jamii
za wabantu zaidi ya makundi mia nne (400) yalienea barani Afrika na kueneza
lugha zao za kibantu kwani ndizo zilizokuwa zikitumika katika mawasiliano. Mfano
nchi kama Nigeria, Kameruni, Guinea ya Ikweta, Gabon, Jamuhuri ya Kongo,
Rwanda, Burundi, Uganda, Kenya na Tanzania jamii zake nyingi zinatumia lugha za
kibantu katika mawasiliano.
Bantustani ni ardhi waliyotengewa Waafrika weusi
wa nchi ya Afrika Kusini wakati wa kipindi cha ubaguzi wa rangi, wakati ambapo
jamii za Afrika Kusini zilivyochangamana na jamii nyingine za kigeni kutoka
Ulaya na Asia.
Negro ni neno lililokuwa likitumika na
watumiaji wa lugha ya kiingereza kumaanisha mtu mweusi, hivyo basi M-Negro ni
mtu mweusi. Kwa ujumla M-bantu na M-negro wote ni watu weusi wenye asili ya
Afrika.
Ushenzi ni hali ya kuwa nyuma kimaendeleo na
kutenda matendo ya kijinga na kikatili au ni hali ya kutostarabika (Kamusi ya
Kiswahili Sanifu).Kwa mujibu wa maana hii ya ushenzi, si kweli kuwa wabantu ni
mishenzi yaani ni watu wasiostaarabika na walio nyuma kimaendeleo. Wabantu
kihistoria inathibitika kuwa na mifumo yao ya kimaisha, shughuli zao za
uzalishaji mali kama vile kilimo, ufugaji na shughuli nyingine za kijamii. Pia
wabantu walikuwa na tamaduni zao, mila na desturi zinazothibitisha kuwa wabantu
hawakuwa washenzi.
Dhana ya fasihi imefasiliwa na wataalam
mbalimbali wa fasihi kwa mitindo na miono yao tofauti, baadhi ya wataalam hao
ni kama vile;
Fasihi ni Sanaa yaani mkusanyiko wa kazi
mbalimbali zilizosanifiwa kwa kutumia lugha itumiayo Zaidi maneno na
kujishughulisha na jinsi binadamu anavyojitambua mwenyewe binafsi, pia anavyoathiriwa na binadamu wenzake aidha na vingine aina kwa aina katika mazingira
mbalimbali ya maisha (Nkwera,
F.V,(2003:94).
Fasihi ni sanaa itoayo maudhui yake kwa kutumia
lugha ya maneno ambayo hutamkwa ama kuandikwa (Senkoro F.E, 2011:11).
Fasihi ni Sanaa ya lugha inayoshughulikia
masuala yanayohusu binadamu matatizo yake, ndoto zake, matumaini yake, migogoro
yake, na jinsi anavyoingiliana na mazingira yake (Wamitila, 2004:19)
Kwa ujumla, fasihi ni sanaa itumiayo
lugha katika ustadi wa hali ya juu na wenye kueleweka katika kufikisha ujumbe kwa hadhira au jamii lengwa, kuburudisha, kuonya,
kukejeri, na hata kukashifu kwa njia ya maandishi au masimulizi. Fasihi kama
sanaa itumiayo maneno, inajenga picha halisi ya mwanadamu katika maisha yake,
mahusiano yake na viumbe wengine, migogoro yake na mazingira, shida zake, raha zake,
matumaini yake na jinsi anavyopiga hatua katika maendeleo yake. Fasihi
bila kujali ni fasihi andishi au fasihi simulizi imekuwa na mchango mkubwa kwa
jamii ya watu mbalimbali na kusaidia jamii hizo au watu hao wasiendelee
kujitukana na kujiita M-BANTU na M-NEGRO kama ifuatavyo;
Fasihi imesaidia kuchochea uzalishaji mali
katika jamii; kutokana na shughuli au kazi mbalimbali za fasihi, fasihi
imesaidia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za uzalishaji mali. Tangu enzi za
ujima fasihi ilitumika Kama nyenzo mojawapo ya uzalishaji Mali. Jamii zilipata
kutumia nyimbo Kama nyenzo mojawapo ya uzalishaji Mali katika shughuli za kilimo,
uwindaji na shughuli nyingine za kijamii. Kwa kuwa fasihi inabadilika kulingana
na mazingira na wakati, fasihi imetoa mchango mkubwa hadi leo katika shughuli
za uzalishaji mali. Kuna nyimbo mbalimbali zinazohamasisha kazi. Kwa mfano
wimbo wa Vijana fungeni mikanda wa
TMK Wanaume Family na wimbo wa Vicky Kamata Wanawake na Maendeleo ni baadhi tu ya nyimbo nyingi zinazo
hamasisha kazi katika jamii.Vile vile methali kama vile Asiyefanya kazi na asile, Mga gaa na upwa hali wali mkavu, haba na haba
hujaza kibaba, ndo ndo ndo si chululu ni mifano ya kazi za fasihi zinasaidia kuhamasisha shughuli za uzalishaji mali
katika jamii za wabantu. Pia katika fasihi andishi, kuna vitabu kama vile Kijiji Chetu, Wasifu
wa Siti Binti Saadi, Nguzo Mama, ni
miongoni mwa kazi za fasihi andishi zinazochochea uzalishaji mali kwa jamii za wabantu. Kwa mifano ya kazi
hizo na nyingine nyingi za kifasihi, ni dhahiri shahiri kuwa fasihi imetusaidia
tusiendee kujitukana kwa kuchochea maendeleo na kujenga jamii yenye misingi ya
kujitegemea katika nyanja mbalimbali za kimaisha.Misingi hiyo katika jamii za
kibantu zinajitokeza katika ngazi ya familia hadi ngazi ya taifa hususani
katika nchi yetu, kwani hadi sasa sera inayotawala bado inachochea shughuli za
uzalishaji mali na kufanya kazi (Hapa kazi tu,)
Fasihi imesaidia katika ujenzi wa jamii mpya
zenye macho na fikra pambanuzi.Fasihi imesaidia kuibua fikra za kimapinduzi
zinazosaidia jamii kuhama katika hali moja hadi nyingine. Uwepo wa kazi
mbalimbali za kifasihi umesaidia kuibua fikra za mapinduzin zinazopinga masuala
ya uongozi mbaya, rushwa, uhujumu uchumi na ukasuku kwa viongozi. Pia kupingaa
fikra kandamizi na za kibaguzi katika jamii. Kwa mfano, nyimbo kama vile Mjomba ya Mrisho Mpoto, Keki ya Taifa ya Wakoloni na Songa, Kikao cha dharura ya profesa Jay, ni nyimbo zinazopambanua maovu katika mfumo wa serikali, na kujaribu kutoa ushauri
juu ya nini kifanyike ili kusawazisha mfumo wa kiutawala kwa kufuata sera ya
utawala bora. Pia katika fasihi andishi, kuna vitabu mbalimbali vya riwaya,
tamthiliya na ushairi vinavyopinga masuala mbalimbali kama vile uongozi mbaya,
rushwa, uhujumu uchumi na mengine mengi yanayokwamisha na kurudisha nyuma
maendeleo ya jamii. Kwa mfano vitabu kama vile Msomi Aliyebinafsishwa, Wasakatonge,
Mabepari wa Bongo, Kivuli Kinaishi na vingine vingi ni
baadhi tu ya kazi nyingi za fasihi andishi zinasawiri mifumo mibovu ya
serikali, rushwa, uhujumu uchumi katika jamii mbalimbali. Hivyo basi kutokana
na kazi hizo fasihi imetusaidia kutoendelea kujitukana wenyewe kwa kuwa na
mifumo mibovu ya kiuongozi na utawala kwa ujumla. Fasihi imetuasa kuachana na
mambo hayo yanayokwamisha maendeleo na kuamua kujenga jamii mpya yenye itikadi
na mambo yanayonufaisha jamii kwa ujumla na wala si watu wachache, kwani tangu
awali wabantu na wanegro walikuwa na mifumo bora ya kiutawala isiyobagua wala
kunyanyasa watu wake.
Fasihi imesaidia kuachana na mila na desturi
zilizopitwa na wakati na zenye madhara katika jamii. Kutokana na kazi mbalimbali
za kifasihi, jamii imeachana na mila na desturi kandamizi na za kibaguzi katika
jamii. Kwa mfano fasihi imesaidia kupiga vita watoto wa kike kuchaguliwa
wanaume wa kuwaoa. Fasihi imesaidia kupiga marufuku suala hilo na kwa namna
moja ama nyingine imeonesha njia ya mafanikio.Kuna nahau kama vie mapenzi majani huota popote, penzi kikohozi
kulificha huwezi, asiyekupenda hakuthamini, ni baadhi tu ya amali za fasihi
simulizi zinapinga hali ya wazazi kuchagulia watoto wao wake au waume wa kuishi
nao kuwa ni makosa. Kila mtu ana moyo na moyo huwa na chaguo lake hivyo ni
vyema moyo ukachagua kile kitakacho furahisha moyo na wala si kuchaguliwa Mfano
katika kitabu cha Vuta N′kuvute
Yasmini anapochaguliwa mume wa kuishi nae na wazazi wake ambaye hakumridhia
kunasasbabisha ndoa hiyo kuvunjika.Pia kuachana na mauaji ya albino, fasihi kwa kupitia nyimbo na tanzu nyingine inapinga
vikali mauaji ya albino au watu kuuana wenyewe kwa wenyewe kwa minajiri ya
kupata pesa na kuwa matajiri. Fasihi inaionya jamii juu ya suala hilo kwani
albino anaweza kuishi na kufanya kazi kama binadamu wengine.Mfano nyimbo ya
Kilimanjaro music Tusiue albino,
misemo kilema nae mtu, usimcheke chongo ni
baadhi ya kazi za fasihi zinazopinga watu kubaguana katika jamii kwa sababu za
kimaumbile, rangi, nasaba zao kwa namna moja ama nyingine. Katika fasihi andishi hali hii ya kupinga mauji ya albino na
ubaguzi kwa ujumla inajidhihirisha katika kitabu cha Takadini. Hivyo basi tunaona namna ambavyo fasihi ilivyoweza
kutusaidia kupinga tamaduni zilizopitwa na wakati kama vile kuua albino,
kuchaguliwa mume au mke wa kuoa, kutowasomesha atoto wa kike na mengine mengi
yanayotufanya tusiendelee kujitukana wenyewe kwa kuwa Wabantu au Wanegro.
Kulinda maslahi ya taifa, fasihi imeonesha
mambo ambayo yanalenga kulinufaisha taifa bila kujali rangi wala kabila kwa
manufaa ya jamii nzima. Fasihi imeweza kukemea matendo maovu yanayofanywa na
baadhi ya viongozi kwa manufaa yao binafsi na kufanya taifa kuwa katika hali ya
umaskini. Mfano katika kitabu cha Msomi
Aliyebinafsishwa mwandishi anaonesha matatizo ya wasomi kupenda kujinufaisha
wenyewe kwa kujilimikizia mali bila kujali taifa. Pia mambo ya uongozi mbaya
ambao haulengi kuwanyonya watu wa hali ya chini. Mfano katika kitabu cha Kisiwa cha Giningi.
Vilevile katika fasihi simulizi, masimulizi
mbalimbali ya zamani yaliyokuwa yanasimuliwa kwa lengo la kufanya watu kulinda
na kupenda utaifa kuliko watu binafsi, nyimbo na matambiko ya kale yalilenga
kujenga mshikamano na kulinga maslahi yao kama jamii moja.Mfano misemo kama
vile, nyumbani ni nyumbani, mkataa kwao
ni mtuwa ni amali za fasihi simulizi zinazohamasihsa kuthamini na kulinda maslahi
ya taifa kwa ujumla bila kuangalia mtu mmoja mmoja. Hii ni ishara kubwa kwamba fasihi imetusaidia tusiendelee kujitukane
wenyewe kwa kujiita Mbantu,Mnegro badala yake kulinda taifa zima dhidi ya
madhira ya dunia kama vile magonjwa kama vile UKIMWI, EBOLA, mafuriko na
mengine mengi.
Fasihi imesaidia kueneza itikadi mbalimali,
fasihi kama sanaa imeweza kueneza itikadi husika kwa kipindi tofauti tofauti.
Mfano katika kipindi cha ukoloni fasihi ilioweza kupinga ukoloni kwa mfano,
methali kama vile Mzungu katupwa
jalalani, misemo kama vile kupe, mabeberu. Amali zote hizo za fasisihi simulizi zilikuwa
na malengo ya kumnyanyapaa mkoloni kwani ni mtu asiye na huruma kwa waafrika.Pia
nyimbo mbalimbali zilitungwa kupiga vita ukoloni kutokana na mabaya yote.
Katika fasihi andishi itikadi za wabantu na
wanegro kwa ujumla bado zimejitokeza kwa namna moja ama nyingine ikiwa ni
kupinga itikadi za kikoloni. Mfano katika vitabu kama vile Mashairi ya Saadan Kandoro, Ubeberu Utakwisha, kinjekitile na
vingine vingi vilivyoandikwa kwa lengo la kupinga itikadi na mifumo ya kikoloni
ambayo iliharibu mifumo ya awali ya wabantu. Hivyo basi, fasihi imetusaidia
kuendeleza itikadi zetu za awali na kufanya tusijitukane wenyewe kwani kutetea
mifumo yetu ya awli ni dhahiri kuwa haikuwa na chembe yoyote ya kibaguzi wala
unyanyasaji kiutawala na kijamii.
Kuhifadhi
amali za jamii;fasihi ni kama ghala la kuhifadhia amali mbalimbali za jamii
yaani tamaduni pamoja na historia ya jamii huika.Katika kuhifadhi amali za
jamii fasihi inakuwa nyenzo muhimu.Aidha wanajamii hufahamishwa kifasihi
historia yao,wao ni nani na wanachimbukia
wapi.Maarifa haya ni muhimu kwa wanajamii hususani wabantu kwani
husaidia sio tu kujielewa bali pia kujitambua.Zipo kazi mbalimbali ambazo
zinaelezea historia ya wabantu kama vile Moto wa mianzi ambayo huelezea
historia ya wahehe,Zawadi ya ushindi
amabayo huelezea vita ya kagera na Kinjekitile.Kuepo kwa kazi hizo za fasihi
inaonesha kuwa wabantu wana historia yao na si
washenzi bali nao wana maendeleo
ambayo yamefikiwa.Fasihi imesaidia kwa kiasi kikubwa wabantu wasiendelee kujitukana
kwa kuwa fasihi inaeleza historia yao vilevile kutunza amali za jamii mbalimbali
za wabantu.Amali za jamii kama vile ngoma,nyimbo,ngonjera,ngomezi na semi
mbalimbali hutunzwa na fasihi katika jamii za wabantu.
Kukuza
na kueneza stadi za lugha za wabantu.kwa kuwa fasihi hutegemea sana katika
lugha hivyo basi semi, hadithi, vitendawili na kuimba hutumia lugha ambazo
miongoni mwazo hutumiwa na wabantu.Fasihi simulizi kwa mfano ina mchango mkubwa
miongoni mwa wabantu katika kuzimiliki stadi za lugha zao.Kutumika kwa lugha za
wabantu katika fasihi inaonesha kuwa wabantu wana lugha zao na wala si washenzi
(watu wasio na maendeleo).kiswahili kama lugha ya wabantu kimekuwa na kuenea
kutokana na fasihi.
Kuunganisha
jamii au vizazi;fasihi imesaidia katika kuunganisha kizazi kimoja hadi kingine katika vipindi
mbalimbali.Kwa mfano hapo awali ushairi wa Kiswahili ulikuwa ukitungwa
kimasimulizi na baadae ukaanza kutungwa kimaandishi miongoni mwa jamii za
watu katika upwa wa Afrika
mashariki.Maendeleo ya fasihi kutoka katika fasihi simulizi hadi katika fasihi
andishi kumeunganisha vizazi vya kale
vya wabantu na vilivyopo na vijavyo.Kutokana na kukuwa kwa Kiswahili kazi
mbalimbali za fasihi kama vile ushairi,tamthiliya na riwaya zilitungwa kwa
kuzingatia utamaduni wa jamii pana.Fasihi ni msingi wa kuunganishia wanajamii(wabantu)waliopo na waliopita kwa
kutambiwa hadithi,methali na nyimbo zao.
Kuongeza
pato miongoni mwa wabantu;Kazi mbalimbali za fasihi zina umuhimu kwa wabantu
kwa sababu husaidia wasiendelee
kujitukana kuwa wao ni washenzi hii ni kutokana
na fasihi huweza kuwasukuma mbele wabantu katika hali ya chini ya
kimaisha mpaka katika hali nzuri ya maisha.Kwa mfano katika
majigambo,methali,mashairi hadithi,vitendawili,nahau,riwaya na tamthiliya ni
kazi za kifasihi zinanozo saidia ili wabantu wasiendelee kujitukana kama wao ni
washenzi.kwa mfano kuna nahau na misemo mbalimbali ambazo ni kichocheo cha
maendeleo katika jamii za wabantu.Kwa mfano “Misitu ni mali” na “maji ni
uhai”.Methali kama vile “haba na haba hujaza kibaba”,”Mtegemea cha ndugu hufa
masikini”,”Ukitaka cha mvunguni sharti uiname”,vilevile kuna kazi kama za
majigambo ambazo huonesha ushujaa katika mambo mbalimbali.kwa mfano wa majigambo;
“Mimi ni,
Mahali-pa-juu.azaae matunda,
Kamba ya kupandia ifikishayo kwenye kilele
Cha mnazi (yaani cheo cha ‘eze’)
Kisu kivunacho pesa
Utajiri kutoka juu
Mgombanaji awagombaniaye nduguze
Mkulima alimaye njaa (Ili kuikomesha).
Majigambo
kama hayo huhamasisha wabanyu katika harakati za kujikwamua kimaisha miongoni
mwao.
Vilevile
kazi za fasihi andishi husaidia katika kuongeza pato. Kwa mfano kuuza vitabu
kama vile vya riwaya,ushairi na tamthiliya husaidia kuongeza pato na kusaidia
kuwaendeleza wabantu katika hali ya kiuchumi.Kuendelea kiuchumi miongoni mwa
wabantu kumesaidia wasiendelee kujitukana kuwa wao ni washenzi bali ni watu
wenye maendeleo yao kama zilivyo jamii nyingine.
Kwa ujumla, fasihi imetusaidia tusiendelee
kujitukana kutokana na ukweli kuwa fasihi inadhima nyingi katika maisha ya kila
siku ya binadamu japokuwa huwa inabadilika kulingana na mazingira na wakati.
Fasihi imesaidia kuainisha vipengele anuai vya kimaisha vinavyotakiwa
kuendelezwa na kuachwa kama vile mauaji ya albino na tamaduni za kale
zilizopitwa na wakati. Fasihi pia imetusaidia kuonya na kuadabisha jamii vile
vile kuelimisha jamii, kwa mfano kuelimisha jamii juuu ya masuala ya UKIMWI
kupitia nyimbo mfano wimbo wa Feruzi ‘starehe’,
masimulizi, nahau na hata misemo mbalimbali ili kujikinga na gonjwa hilo la
hatari.
Marejeleo.
Amatu.J.K
,(2003),Fasihi Simulizi.Mvule Africa
Publsher:Nairobi
Kabuta.N.S
,(1197),Isimu-Ushairi:Muundo wa majigambo.University
of Genk:Genk
Maitaria.J.N,(2003),Methali kama formula katika utunzi wa
uwasilishaji wa ushairi wa Kiswahili.Chuo kikuu cha Kenyatta:Nairobi.
Msuya A.B (2008).Semi, Maana na Matumizi. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo
kikuu cha Dar es salaam.
Sengo T.S (1992) Tungo za Pwani.Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam.
Senkoro F. E (2011).Fasihi. Kautu Limited. Dar es Salaam.
TUKI,(2005),Kamusi ya Kiswahili.Oxford university
press:Dar es salaam.
Wamitila K.W (2004).Kichocheo cha Fasihi Siulizi na Andishi. Focus Publishers ltd.
Nairobi.
TANBIHI; Makosa ya kiothografia yatakayojitokeza katika makala hii ni makosa ya kiuchapishaji na siyo ya vyanzo vilivyorejelewa.