Jumanne, 16 Juni 2015

VIPENGELE VYA FANI KATIKA TAMTHILIYA YA KIVULI KINAISHI



Katika makala hii tumeanza kwa kueleza dhana ya fani kisha tukatazama maana ya tamthiliya kulingana na wanazuoni mbalimbali, kisha tukagusia chimbuko na maendeleo ya tamthiliya kwa kifupi na mwisho tumejadili vipengele mhimu vya fani katika tamthiliya ya Kivuli Kinaishi iliyoandikwa na Said Mohamed.
 Kwa kuanza na dhana ya fani.
Fani ni ufundi katika kuumba umbo la kazi ya fasihi kutokana na ubunifu wake. Fani hujuisha muundo, mtindo, matumiziya lugha wahusika na mandhari (www.mwanchi.co.tz/makala/vipengele mhimu vya uhakiki wa kazi ya fasihi).
Fani ni ufundi wa kisanaa anaoutumia msanii katika kazi yake. Ni ustadi au ubingwa au mbinu ambazo msanii wa kazi ya fasihi hutumia katika kuwasilisha ujumbe wake kwa hadhira yake.(Senkoro 1982:8)
Fani ni sanaa, ni jumla ya vipengele vya lugha vilivyowekwa katika mpangilio mahususi ili kutoa kwetu maana Fulani (Mulokozi na Kahigi 1978:53).
Kwa ujumla, fani ufundi au ujuzi wa kisanaa atumiao mwandishi au mtunzi wa fasihi katika kufikisha ujumbe kwa jamii/hadhira iliyokusudiwa. Fani ni kipengele pekee ambacho humtofautisha kati ya msanii mmoja na mwingine, mfano wa vipengele hivyo ni matumizi ya lugha, mtindo, muundo, mandhari, na hata ujuzi wa wahusika.
Tamthiliya ni mchezo wa kuigiza au utungo wa kisanaa ambacho huweka wazo Fulani katika matendo na mazungumzo (Nkwera h.t.chombez.blogsport.com/2013/11/tmthiliya.htm/?.m=1)
Tamthiliya ni utungo wa kisanaa ambao huweka wazo Fulani katika matendo na mazungumzo (Tuki 2004).
Tamthiliya ni utungo wa fasihi ambao hubuniwa, kwa kiasi kikubwa kwa lugha ya mazungumzo yenye kuzua na kuendeleza matukio ya hadithi ya utungo huo. Chanzo cha matukio ya hadithi ya tamthiliya mara nyingi hupatikana humohumo katika mazungumzo ya wahusika wake  (Mazrui na symbo 1992). Mlokozi (1996) anasema hadithi ya tamthiliya husonga mbele kwa njia ya vitendo na mazungumzo ya wahusika. Hivyo anaonyesha bila wahusika hata mazungumzo hayatakuwepo. (chombez.blogspot.com/2013-11-01-achieve).
Kwa ujumla, tamthiliya ni andiko la kiuigizaji linalotoa simulizi kwa kuonyesha maneno na matendo. Hii inamaana kwamba tamthiliya ni utanzu ambao hauna msisitizo wa kuigizwa jukwaani ukilinganisha na drama na pia tamthiliya lazima ikidhi vigezo vya kidrama kwasababu isipokidhi inakuwa chapwa yaani haina shauku. Vigezo vya kidrama ni kama vile muonekano dhahiri wa jukwaani, mwonekano dhahiri wa hisia, usikiaji wa ngoma, ishara na matendo, ushiriki wa moja kwa moja wa hadhira na usikiaji dhahiri wa sauti za binadamu, ndege au wanyama.
Fasihi ya majaribio au tamthiliya ya majaribio ni fasihi iliyo lenga kuleta upya katika fasihi ya Kiswahili. Watunzi wengi wa tamthiliya ya Kiswahili walikuwa wakitunga kazi zao kwa kuiga mbinu mbinu na kanuni za tamthiliya ya ulaya. Kuanzia miaka ya 1970 watunzi wa tamthiliya ya Kiswahili hawakuridhika na uigaji huo. Waliona kuwa kuna umuhimu wa waafrika kuwa naTamthiliya yao yenye kuchota mbinu zake kutokana na sanaa za jadi za kiafrika. Lengo kubwa lilikuwa nikufanya Tamthiliya ioane na utamaduni na mazingira ya kiafrika(Mlokozi 1996).
Kwa mjibu wa Senkoro (2011:62-63) anaeleza kuwa majaribio mengi yanayofanyika katika Fasihi ya Kiswahili yanaelekea kuwa yamechota kutoka katika fasihi simulizi ya Kiswahili.
Kwa ujumla, Tamthiliya ya majaribio ni aina ya Tamthiliya ambayo hutumia mbinu na taratibu ambazo hazijazoeleka katika kumbo la kawaida la Tamthiliya, hii inamaana kwamba vipengele mbalimbali vya fani na maudhui ambavyo vilichukuliwa kutoka katika fasihi simulizi vikaingizwa katika tamthiliya ya Kiswahili ya majaribio ili kuonyesha utofauti uliopo kati ya Tamthiliya ya kiafrika na kimagharibi.
Hapo mwanzo kabla ya kuibuka kwa Tamthiliya ya Kiswahili ya majaribio hapa kwetu Afrika kulikuwa aina tofauti za sanaa za maonyesho kama vile utambaji, ngoma, miviga na sherehe ambazo zilikuwa na sifa zifuatazo: Zilitungwa hapo hapo, hazikuandikwa, hazikuwa za biashara, zilifanywa kwenye duara, hadhira na watendaji walibadilishana nafasi na sanaa iliyokamilika haikuwa ya mtu mmoja bali ya jamii nzima.
Baada ya ujio wa tamthiliya za kimagharibi umbo lake lilitofautiana na sanaa za maonyesho za asili kwani zilikuwa na mambo yafuatayo: Maandishi, waigizaji, hadhira, ukumbi, jukwaa, matapo, mgawanyo dhahiri wa majukumu(kazi), zilikuwa za biasharana zilikuwa mali ya mtu mzima. Hivyo waandishi wengi wazawa walianza kuandika kazi zao za tamhiliya kwa kufuata kanuni za uandishi wa kiaristotle.
Kuanzia miaka 1970 watunzi wa tamhiliya ya Kiswahili hawakuridhika na uigaji wa tamthiliya za kimagharibi(kiaristotle). Hivyo waliona kuwa kuna umuhim wa waafrika kuwa na tamthiliya yao yenye kuchota mbinu zake kutoka katika sanaa za jadi za Kiafrika. Lengo kubwa ilikuwa ni kuifanya tamthiliya ioane na utamaduni na mazingira ya kiafrika.(Mulokozi 1996).
Kwa kutumia mifano kutoka katika Tamthiliya ya KIVULI KINAISHI ya Said Mohamed    vipengele mhimu vya kifani vinavyojitokeza katika tamthiliya ya Kiswahili ya majaribio ni kama vifuatavyo:
Mtindo, ni jumla ya mbinu au sifa zinazomwezesha msanii kuwasilisha ujumbe wake au kuelezea msanii anavyounda kazi yake(Wamitila 2003). Katika kipengele hiki cha mtindo wasanii wengi wa tamthiliya ya Kiswahili ya majaribio huchanganya tanzu mbalimbali za kisanna kama vile nyimbi, ushairi na hadithi. Mfano, katika  tamthiliya ya KIVULI KINAISHI iliyoandikwa na Said Mohamed imechanganya tanzu mbalimbali kama nyimbo na hadithi. Mfano katika onyesho la nne.(uk.31) mwandishi ametumia wimbo anasema;
“NYIMBO: Nasikia parakacha myembeni
    Kam mshambigija mleteni

            Eee wewe … eee wewe
  Kupeana ni kikoa,
     Toa name nitoe
       Ati kupeana ni kikoa
     Toa name n’toe!”
 Utanzu mwingine alioutumia katika Tamthiliya hii ni hadithi mfano katika onyesho la kwanza (Uk10) msanii anasema ;
                        “Bi.kizee;  Haya(anaingia hadhira huku anavuta ugoro na huku
                                           anapakasa ukili wake- kaketi kijamvini) paukwaa….
                          Wtoto na
                           hadhira:    kimya
                           Bi. Kizee:  paukwa…….
                           Watoto na
                           hadhira;    kimya
                           Bi. Kizee:  paukwa…itikieni….itikieni basi….
                           Watoto na
                           hadhira;     Pakawa….”
Kwa hiyo mbinu hii ya kuchanganya tanzu katika kazi moja ya fasihi husaidia hadhira kuvutiwa na kuhamasisha kwa wasomaji kutokana na kuoana na utamaduni wao.
Vilevile methali zimeweza kujitokeza katika( Uk.24) anasema,
“unachumia juani na kulia kivulini, (Uk.67) kikulacho kinguoni mwako, (Uk.111) majuto ni mjukuu, (Uk.6) kuishi  kwingi kuona mengi na kujua mengi pia”.

Muundo ni mpangilio wa kiiufundi anaoutumia msanii katika kazi yake(Senkoro F.E.M.K(1982). Kwa ujumla muundo ni mpangilio na mtiririko wa kazi ya fasihi simulizi kwa upande wa visa na matukio, muundo hujumuisha jinsi msanii wa kazi ya fasihi alivyofuma, alivyounda na anavyounganisha tukio moja na lingine, kitendo kimoja na kingine wazo na wazo, sura moja na nyingine, ubeti na ubeti, hata mstari wa ubeti na mwingine. Mfano katika tamthiliya hii ya KIVULI KINAISHI kuna visa viwili nadi ya kisa kimoja yaani kisa cha Bi kizee na watoto na kisa cha maisha ya Giningi. Vilevile mwandishi ametumia Mianzo na miishio ya kifomula mfano, mianzo ya kifomula(Uk10) msanii anasema:
                                 “Bi.kizee; Haya(anaingia hadhira huku anavuta ugoro na
                                                  huku anapakasa ukili wake- kaketi     kijamvini) paukwaa….
                                   Wtoto na
                                   hadhira:       kimya
                                   Bi. Kizee:    paukwa…….
                                   Watoto na
                                   hadhira;       kimya
                                   Bi. Kizee:    paukwa…itikieni….itikieni basi…
                                   Watoto na
                                   hadhira:      pakawa….”
Pia ametumia miisho ya kifomula mfano, ukurasa wa mwisho kabisa (Uk130) onyesho la 10 mwandishi anasema;
           “ Bi.kizee: Basi huo watoto ndio mwisho wa hadithi…na kama mwisho wa hadithi ulivyo
                           Huwa furaha au huzuni”
Kutokana na kipengele hiki cha mianzo na miisho ya kifomula katika Tamthiliya ya kiswahili majaribio kimeleta upekee kwa sababu huvuta umakini wa hadhira kuwa na shauku ya kutaka maudhui ya Tamthiliya, na hii ni kutokana na maneno anayotumia msanii katika kuanza kazi yake.
Matumizi ya lugha, ni namna ambayo msanii ameteua na kupangilia tamathali za sema kama sitiari,tashbiha, takriri, tashihisi, tafsida, methale, misemo, nahau, taswira na lugha za kigeni (Senkoro F.E.M.K 1982). Katika Tamthiliya ya “KIVULI KINAISHI” iliyoandikwa na Said Mohamed. Mwandishi ametumia taswira mbalimbali kama ifuatavyo: KIVULI KINAISHI ni taswira inayo maanisha mawazo ya kimpinduzi yaliyokwisha pandikizwa na kwa vizazi vipya ili kudai haki na usawa. Taswira nyingine ni “unga wa rutuba” (uk112) yenye maana ya elimu ya kujitambua katika jamii na kutambua nafasi yako na kuwa na uwezo wa kuwaelimisha wengine.
”Bi.kirembwe: Enh! (anashituka….anashangaa) umebwia nini?
  Mtolewa: unga wa rutuba…..
   Bi.kirembwe: unga wa rutuba……a-a-a-a-a-mbaya…..mbaya
   Mtolewa: Ndiyo…………”
Taswira nyingine ni “unga wa ndere” wenye maana ya itikadi zinazomfanya mtu katika tabaka tawala akubalike na kushika miiko mfano (Uk.111) Mtolewa anasema:
           “Mtolewa: Mtolewa wa leo hayupo pamoja na wewe … yuko
                             maili elfu na moja mbali na wewe. Mtolewa wa
                              leo hasimamii mamlaka uliyompa, anasimamia
                              mamlaka ya hawa wote   waliopewa unga wa ndere..”
 Taswira nyingine ni mdundo wa ngoma unaomaanisha kitendo cha kufuata mashariti kama tabaka tawala litakavyo (Uk.31) katika onyesho la nne.
                                   “Kumbwaya, ugoma maarufu wa Giningi, analia, kabla
                                     pazia kufunguliwa.Nyimbo nyimbo inakuja na ngoma inaimbwa
                                     kwa sauti za kike kwa kiume, za wakubwa kwa wadogo:
                                     Pazia linafunguliwa kidogokidogo kuwaridhisha wari
                                     Wanaotaka kuingizwa giningi.”
vilevile mwandishi ametumia takriri katika onyesho la nane (uk.111) anasema,
          Bi.kirembwe: “Ulumbi …ulumbi… uluumbi (anakwenda huku akirudi huku)
                                 Umechomoka Mtolewa, majuto hakika ni mjukuu
                                  nilihisi mimi tokea mwanzo,lakini sijui kanini sikuchukua hatua?”
Hivyo kipengele hiki cha lugha  katika Tamthiliya za kimajaribio kimeweza kuleta upya katika kazi za fasihi kwa kuingiza vionjo asili vya kiutamaduni na  kuepusha migogoro ya moja kwa moja kati wasanii na tabaka tawala kwa kutumia lugha ya mficho kwa kutumia taswira.
Wahusika, ni binadam wanaopatikana katika kazi ya fasihi ambao wana sifa za kimaadili, tabia, kiitikadi na falsafa ambazo hutambulishwa na wanayoyasema na wanayoyatenda.(Wamitila 2002). Katika tamthiliya wahusika hujidhihirisha katika utambaji mfano, katika Tamthiliya ya KIVULI KINAISHI iliyoandikwa na Said Mohamed amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwashirikisha hadhira katika utambaji. Mfano (Uk.60) onyesho la tano mwandishi anasema:
Mtangazaji: Mpo? Wali mpo?
Wali wote: tupooo!
Mtangazaji: yote sawaaa?
Wali wote: yote sawa…sawa….sawa…
Vilevile amefanikisha kuwashirikisha hadhira (Uk10) msanii anasema,
             Bi. Kizee:  paukwa            
             Watoto na
             Hadhira:  Pakawa….
Hivyo basi ushirikishwaji wa hadhira ni muhimu kwa sababu huipa Tamthiliya uhai, mvuto na kuondoa uchovu kwa hadhira.
Mandhari, ni sehemu ambayo matukio ya hadithi au masimulizi hutokea.mandhari huweza kuwa halisi kama vile njiani, msituni, kijini mjini au ya kufikirika kama vile kuzimu, peponi na mbinguni(Senkolo F.EM.K.1982). Vilevile mandhari ni elementi ambayo hutufichulia wapi na lini ambapo matukio Fulani yalifanyika(Wamitila 2002).mwandishi anaweza kutumia mandhari halisi nay a kuonekana au mandhari ya kufikirika. Mfano katika tamthiliya ya KIVULI KINAISHI mwandishi ametumia mandhari halisi ya kitanzania kutokana na kutaja kwa miji kama vile unguja na pemba vile vile mambo kama rushwa, uongozi mbaya na hali ngumu ya maisha vinaashiria nchi za dunia ya tatu kama vile Tanzania ambapo baadhi ya viongozi hutumia madaraka yao vibaya. Vilevile kuna mandhari ya kubuni katika onyesho la tisa (uk.117)mwandishi anasema,
“BI KIREMBWE: Na sauti hiyo inatoka wapi?
SAUTI: Kuzimu…..
BI KIREMBWE: Aha, sasa naanza kuelewa… sauti hiyo ni sauti ya Mtolewa 
                             inayotoka  kuzimu...”
Hivyo mandhari huifanya kazi ya fasihi kuendana na uhalisia hasa mandhari halisi.
Kwa ujumla vipengele hivi ndivyo hutofautisha Tamthiliya ya Kiswahili ya majaribio na kuipa upekee ukilinganisha na Tamthiliya zilizotungwa kabla ya miaka 1970s ambazo zilikuwa na mlengo wa Tamtiliya ya kimagharibi ambapo watunzi wa Tamthiliya hawakurithika na uigaji huo, wakaona kunaumhimu wa waafrika kuwa na Tamthiliya yao yenye kuchota mbinu zake kutokana na sanaa za jadi za kiafrika.
            

                          


MAREJELEO
Faustine, S. (2015) Tamthiliya ya Kiswahili Chuo Kikuu cha Dodoma:  (Hakijachapishwa.)
Mohamed, S. (2009) Kivuli Kinaishi: Oxford University Press, East Africa ltd. Nairobi.
Mlokozi, M.M (1996) Fasihi ya Kiswahili: Taasis ya Uchunguzi wa Kiswahili; Chuo Kikuu cha Dar- es- Salaam.
nkwerah.t.chombozi.blogspot.com.n/2013/11/tamthiliya.htm/?.m=1
Nyangwine, N.& Masebo, J( 2007) Fasihi kwa ujumla. Nyambari Nyangwine Publisher: Dar- es-Salaam.
TUKI (2004) Kamusi ya Kiswahili Sanifu: Chuo Kikuu cha Dar-es- Salaam.
www.mwananchi.co.tz/makala/vipengele muhimu vya uhakiki wa kazi ya fasihi.
Senkoro, F.E.M.K (2011) Fasihi Dar- es- Salaam University Press: Dar- es- Salaam. 












Maoni 4 :