Jumapili, 10 Mei 2015

FASIHI; TAMTHILIYA

      MAANA NA AINA ZA TAMTHILIYA

Na Mwl. Kagita


TAMTHILIYA
Kwa kuanza na maana ya tamthiliya imeelezwa na wataalamu mbalimbali kwa namna tofautitofauti kulingana na vigezo walivyovizingatia.
Mwenda Ntarangwi, (2002:169) anaeleza kuwa, neno tamthilia limetokana na kitendo “mithilisha” ambacho maana yake ni kufananisha au kumithilisha hali ya maisha fulani kwa vitendo. Akahitimisha kwa kusema tamthilia ni maigizo ya matukio au visa fulani kwa uhalisi wake kwa ajili ya kuyasawili maudhui au maelezo fulani. Ubora unaojitokeza katika maana hii ni kuzingatia vipengele vya uigizaji, tukio, suala la kuhusianisha na jamii na kubeba maudhi Fulani.
Udhaifu wa maana hii ni kutozingatia kipengele cha ubunifu pia hakueleza hayo maigizo yanatakiwa yawe ya namna gani ili yaitwe tamthiliya.
 Wamitila, (2002:7) ameeleza kuwa, neno  tamthiliya kwa upana wake linatumiwa kujumuisha maneno drama na play ya Kiingereza. Kwa hiyo, tamthiliya ni utungo unaoandikwa kwa mtindo wa mazungumzo. Ubora wa fasili hii imezingatia kipengele cha mazungumzo ambacho ni kipengele muhimu katika tamthiliya.
Udhaifu wa fasili hii kwanza amechanganya dhana ya tamthiliya na drama ambazo ni dhana mbili tofauti. Kwani tamthiliya msisitizo wake upo katika maandishi lakini drama msisitizo wake upo katika uigizwaji jukwaani. Pia si kila mazungumzo ni tamthiliya. Kigezo cha mazungumzo pekee hakitoshi kuamua utungo fulani kuwa ni tamthiliya.
 Penina Mlama, (1983:203) akirejelewa na Mulokozi, (1996) anasema tamthiliya ni sanaa za maonyesho; sanaa ambayo huwasilishwa ana kwa ana, tukio fulani kwa hadhira kutumia usanii wa kiutendaji. Katika fasili hii Mlama amezingatia vipengele vya sanaa, uonyeshaji, hadhira, utendaji na tukio.
Udhaifu wa maana hii ni kuwa si lazima tamthiliya iigizwe jukwaani; vilevile fanani na hadhira si lazima wawe ana kwa ana. Mfano katika tamthiliya ya “Kivuli Kinaishi” “Ngoma ya Ng’wanamalundi”, “Lina Ubani” na nyinginezo, fanani na hadhira hawapo ana kwa ana.
Udhaifu wa fasili hii Mlama hakuweka wazi urefu huu kuwa ni urefu wa kurasa nyingi au urefu wa tukio linalosimuliwa. Pia si kila hadithi inayosimuliwa jukwaani ni tamthiliya. Kwani hata misikitini na makanisani wahubiri husimama juu ya mimbari kuhutubia waumini wao. Je, hiyo ni tamthiliya? Jawabu ni kuwa hiyo siyo tamthiliya.
Sanjari na hao Mulokozi, (1999:188) anasema kuwa tamthiliya au drama ni fani ya fasihi iliyokusudiwa kutendwa jukwaani kwa ajili ya hadhira fulani. Ubora unaopatikana katika maana hii ni kwa kuwa imezingatia utendaji, jukwaa, hadhira, kusudio na fani inayotendwa. Kwa upande wa udhaifu, maana hiiimechanganya dhana ya tamthiliya na drama. Lakini kwa kiasi kikubwa maana hii inaonekana kukidhi vigezo vingi.
Tunakubaliana na Mulokozi (1996) kuwa sifa walizotoa Mlama na Balisidya kuwa tamthiliya huwa na sifa za kawaida za sanaa za maonyesho. Sifa hizo ni dhana inayotendeka, mtendaji, uwanja wa kutendea, na watazamaji. Hivyo sifa hizi hazitoshi kupambanua sanaa ya maonesho; kwa sababu kuna matendo mengine ya kijamii ambayo yana sifa hizo. Mfano matambiko, hotuba zinazotolewa na watu mbalimbali. Mulokozi alisema sanaa za maonesho ni tukio lenye sifa saba ambazo ni dhana inayotendwa, uwanja wa kutendea, watendaji, hadhira, kusudio la kisanaa, muktadha wa kisanaa na ubunifu.
Kwa jumla tunaifasili tamthiliya kuwa ni utanzu wa fasihi unaotumia lugha ya majibizano yenye ubunifu wa hali ya juu ikiwa haina msisitizo wa uwasilishaji wake jukwaaani ili kufikishalengo mahususi  kwa hadhira iliyokusudiwa kwa njia iliyoandikwa au isiyoandikwa.
Kutokana na kuwa dhana ya tamthiliya inachanganywa na maana ya drama ni vyema tuelezee maana ya drama. Kwa mujibu wa Wamitila, (2003:36) anasema kwamba drama ni aina ya utanzu wa fasihi ambao kimsingi hudhamiriwa kuigizwa mbele ya hadira. Inaweza kuwa imeandikwa au la.
Kwa jumla dhana ya drama inarejelea utungo wa kisanaa unaotumia lugha ya majibizano na matendo yenye ubunifu wa hali ya juu yanayotendwa jukwaani mbele ya hadhira ili kufikisha lengo mahususi kwa hadhira iliyokusudiwa.
SIFA ZA TAMTHILIYA
·        Utoshelevu Kimuundo. Tamthiliya nzuri huwa na sehemu tatu muhimu: Mwanzo, Katikati na Mwisho. Sehemu zake zinatazamiwa kuingiliana, kujengana na kukamilishana.
·        Tamthiliya huwa na lengo. Katika zama za Aristotle, kwa mfano, tanzia ziliwajibika kuzindua hofu na huruma.
·        Vitendo vyote vinavyofanyika katika tamthiliya vinapaswa kuchangia katika ufanisi wa dhamira za mtunzi.
·        Kifani, tamthiliya hutumia mbinu za kisanii zinazowishi wasomaji au watazamaji kuendelea kusoma au kutazamia matokeo ya matendo yanayoigwa. Mbinu hizo ni pamoja na jazanda, kejeli, ritifaa, tashbihi, tashihisi na uzungumzi nafsia.
·        Wasanii bora wa tamthiliya ni wale wanaotunga tamthiliya zinazozungumzia kadhia zinazoweza kutimia katika maisha ya binadamu.

UHALISIA MAZINGAOMBWE
Uhalisia mazingaombwe ni dhana ambayo imeanza kutumika  miaka ya 1920, ambapo mjerumani Franz Roh ndiye aliyevumbua matumizi ya Magical realism mnamo mwaka 1925 ili kuelezea kazi ya mtindo wa ulaya enzi hizo. Roh alilibuni neno hili  ili kuelezea michoro iliyo na uhalisi kama wa picha na kamera. Michoro hiyo ilichanganya mambo ya uhalisi na yasiyokuwa na uhalisi.Baadaye dhana hii ya Uhalisia Mazingaombwe  ilitumiwa na Arturo Urslar kutoka Venezuela alipokuwa anahakiki kazi mbalimbali za wanafasihi wa Marekani ya Kusini waliokuwa wanatumia mtindo huu katika kazi zao. Baadaye Uhalisia Mazingaombwe ulianza kutumika kama nadharia ya uchambuzi wa kazi za kifasihi.
Katika fasihi ya Kiswahili wataalamu mbalimbali wanaeleza kuwa, Uhalisia mazingaombwe ni mtindo uliokuwa ukitumika muda mrefu hata kabla ya taaluma ya uandishi. Mtindo huu ulitumika katika fasihi simulizi na baadae ukatumika katika fasihi andishi. Wanaotumia mtindo huu katika fasihi andishi wanarudia au kufufua kitu ambacho kilikuwepo zamani. (Senkoro2007:11)
Dhana ya uhalisia mazingaombwe imefasiliwa na wataalamu mbalimbali kama ifuatavyo;
Wamitila (2003 a:274), anaeleza kuwa ni mtindo wenye sifa za kuyaelezea matukio ya kifantasia,  kiajabu, au kiuchawi kwa namna ya moja kwa moja inayofanya yaonekane ya kawaida tu.
Faustine, S akimrejelea Methew, S. (1999:267) anasema, Uhalisia Mazingaombwe ni yale mambo ambayo hutokea pale ambapo mandhari na matukio halisi yanavamiwa na jambo ambalo ni la ajabu mno na ni vigumu kuaminika.
Kwa jumla, fasili zote zimegusia uhalisia mazingaombwe kama mbinu ambayo mambo ya ajabuajabu, uchawi, na yasiyo ya kawaida kutokea sambamba na yale yaliyozoeleka katika ulimwengu halisi tuujuao na kuuishi. Katika mbinu hii mazingaombwe hujitokeza  kupitia wahusika, mandhari, motifu ya kisafari na matukio kama misingi mikuu ya uchambuzi wa nadharia hii ambamo ndani yake kumefichwa taswira, ishara na sitiari  zinazohusiana na maisha ili kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa jamii.
Uhalisia Mazingaombwe huwa na sifa kama vile; matukio ya kustaajabisha, motifu ya kisafari, matumizi ya taswira na ishara kwa kiasi kikubwa ambayo hujengwa kutokana na matukio, wahusika  na mandhari. Vilevile mbinu hii hutumika ili kuwakilisha kitu au jambo fulani.
Athari ya mbinu hii inajitokeza katika kazi za waandishi wa mwanzo wa fasihi ya Kiswahili hasa Shaaban Robert na kazi za “Kusadikika” na “Adili na nduguze”.Katika kazi hizi masuala ya safari yanajitokeza kwa kiasi kikubwa, safari siyo jambo la ajabu katika ulimwengu halisi wa maisha japo baadhi ya masaibu yaliyowafika wasafiri waliomo katika kazi hizi ni vigumu kuyaamini katika ulimwengu halisi kwani yamefungamanishwa na uajabuajabu mno. Huo uajabu ndiyo uliofanya kazi hizi na zilizofuatia baadaye kama “Babu alipofufuka” na “Mzingile” kudaiwa zimetumia mbinu za uhalisia mazingaombwe katika kueleza ukweli na hali ya maisha ya jamii walizokusudia waandishi wa kazi hizo
            Udhaifu wa uhaalisia mazingaombwe katika kazi ya fasihi.
Kuhusisha wahusika wakuu walio na akili zisizo timamu, mwingiliano-matini uliopindukia na utambulisho wenye kutetereka.
Umefungwa kwa minyororo ya lugha, na hivyo basi hauwezi kuondoa udhaifu wa lugha katika kuweza kuwakilisha hali halisi kikamilifu.
UCHOTARAISHAJI
Uchotaraishaji au fasihi ya Kiswahili ya majaribio, ni fasihi  ambayo imechota vipengele vya fasihi simulizi ya Kiswahili na kuviweka katika fasihi andishi ya Kiswahili, kwa lengo la kuleta vionjo vipya katika fasihi ya kiafrika. Dhana ya uchotaraishaji inarejelea kufufua fasihi asili ya Kiswahili kwa kutumia mbinu na vipengele vya fasihi simulizi katika tanzu za  fashi andishi kama vile riwaya, ushairi na tamthiliya.
Uchotaraishaji ulifanywa mwanzoni hapa Tanzania na waandishi maarufu wa tamthiliya ya kiswahili kama vile, Ebrahim Hussein na Penina Muhando.  Ebrahim Hussein alitumia mbinu hii katika tamthiliya yake ya Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi, na Penina Muhando katika tamthiliya yake ya Lina Ubani.
Baadhi ya sifa za uchotaraishaji  ni;
Mtambaji, sifa hii hujitokeza katika fasihi ya Kiswahili ya majaribio. Katika tamthiliya ya Lina Ubani, mbinu hii ya utambaji imejidhihirisha, pale ambapo mtambaji anasimulia hadithi ya Bibi.
                       Mtambaji:   Paukwa
                       Hadhira :     Pakawa
                       Mtambaji: Hapo zamani za siku hizi, palitokea huyo Bibi kama mnavyomuona...............…(uk 2)
Matumizi ya taswira na ishara, mbinu hii hutumiwa katika fasihi simulizi kuwasilisha wazo kwa hadhira iliyokusudiwa. Dhana hii imetumiwa katika tamthiliya ya Lina Ubani, ambapo mwandishi ametumia taswira ya zimwi, kuashiria utawala wa mabavu wa aliyekuwa rais wa Uganda  Nduli Idd Amin, kama anavyosema Mtambaji;
             .......Mwisho Zimwi likaamua fujo kuzifanya asubuhi na mapema,ukingoni mwa msitu lilisimama,likapiga makelele kuteremsha ardhi.(uk 18).
Wahusika, na majina,  katika tamthiliya ya Lina Ubani, wahusika waliotumiwa ni Binadamu wenye majina halisi ya kiafrika, wahusika kama Bibi, Huila, Mwana Hego, Mota pia Mhusika Zimwi ambaye katika jamii za kiafrika huashiria ubaya.
Mwingiliano wa  tanzu, (utomeleaji). Mbinu hii imejitokeza katika  fasihi simulizi ambapo vipengele vya fasihi simulizi  huingiliana katika utumizi.  Katika tamthiliya ya Lina Ubani, kuna hadithi ndani ya tamthiliya pia matumizi ya wimbo ambao umeambatanishwa na utambaji. Bibi amekaa analia kwa kuimba na kuomboleza, licha ya hivyo wimbo wenyewe uko katika lugha ya jadi ya Kiafrika na una tafsiri yake kwa Kiswahili.
                             Ing’oma ii sikuidaha doo ae                 Ngoma hii siwezi Oooh!
                              Woi doo ae aya
                             Nimemwitunda dya mele do                 Nisimame juu ya mlima wa Mele
                             Ninange main a baba do                       Niite baba na mama     (uk 1-3)

Mianzo na Miisho ya kifomula, hii ni sifa ya kimsingi katika hadithi za fasihi simulizi ya kiafrika ambapo fanani huanza kuhadithia kwa kuweka viashirio maalumu kwa mfano, fanani husema ;
                          Fanani :Paukwa
                          Hadhira:Pakawa
Katika tamthiliya ya Lina Ubani,mwandishi  ameanza kwa kuelezea hadithi yake kwa mianzo  kama ya hadithi ya fasihi simulizi,kwa mfano
                        Mtambaji :  Paukwa
                         Hadhira:     Pakawa
                         Mtambaji:
         Hapo zamani za siku hizi…………………(uk-2).      Mwishoni Mtambaji amemalizia kwa kitendawili ambacho anaomba hadhira impe mji ili kumalizia hadithi yake mfano Mtambaji:
                                  Akaa! 
                                    Mwenyewe bibi kajifia
                                   Hadithi hakumalizia
                                    Mkitaka nimalizie mimi
                                    Nipeni mji
                                   Lakini mji wenyewe
                                   Usiwe na uvundo
                                  Kwa sababu ubani wa uvundo
                                   Mie siujui.


TANZIA-RAMSA
Ni tamthiliya inayochanganya vipengele vya tanzia na ramsa, hutumiwa sawa na tamthiliya za kibwege - hii ni tamthiliya ambayo inaonyesha kwamba kicheko au furaha ndiyo jibu pekee la maisha kwa watu ambao hawana imani na maisha ambayo kwayo misingi thabiti ya maisha imeondolewa. Mfano tamthiliya ya  Amezidi ya S.A Mohamedi
Tanzia-ramsa ni tamthilia ambayo huonyesha mabadiliko ya aina fulani yanayogeuza mwelekeo wa matukio ya kitanzia na kuufanya kuwa tofauti au wa kufurahisha. Hali hii inaweza kupatikana kwa kuwepo kwa hasidi au mui anayetubu na kuyajutia makosa au msimamo wake au kuwepo kwa mandhari ya kiulimbwende.
Kimsingi, tanzia-ramsa ni tanzia inayoishia kwa furaha. Kinyume chake ni futuhi zimbwe. Dhana hii inaakisi kwa kiasi kikubwa baadhi ya mitazamo ya kidhanaishi ya fasihi ambapo ushujaa na tanzia havijitokezi katika hali ya kawaida kama vilivyozoeleka.
Hali hii inadhihirika katika tamthiliya kama vile ‘The Cherry Orchard’ (Anton Chekhov, 1904), ‘The Winter’s Tale’ (William Shakespeare, 1611).
FUTUHI/KOMEDIA (COMEDY)
Futuhi au komedia ni utungo ambao unachekesha na kuchangamsha. Tamthiliya ya aina hii inaweza kusawiria picha halisi katika maisha  kwa undani ikitumia dhihaka na kejeli kwa kuchekesha. Futuhi huficha ukali wa masuto kadri inavyoendelea kuburudisha hadhira yake.
Futuhi hulenga kurekebisha tabia zinazozidhihaki au zinazozicheka. Kusema futuhi inafurahisha haina maana kuwa dhamira yake haina uzito, kwani huzungumzia masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa njia ya kuchekesha. Futuhi huweza kuwa na sifa zinazotofautiana – jambo ambalo hutumiwa kama kigezo cha kuainisha aina mbalimbali. Lakini vyovyote iwavyo, futuhi hujikwepesha na masuala ya kutia hofu au kushtua.
Athari ya futuhi (kuchekesha) hutokana na matendo, mienendo ya wahusika na hitilafu au ila za kuingiliana kwa kiusemi. Futuhi huwa na viwango mbalimbali vya kuchekesha.
Kwanza, kuna kiwango hafifu (duni) ambacho huhusishwa na futuhi ya chini. Kuna baadhi ya kazi ambapo kiwango cha kuchekesha huwa kigumu kutambulikana na huhitaji utambuzi mpevu. Hii ni sifa ya aina ya futuhi iitwayo Futuhi ya Juu.
Aina zingine ni pamoja na, futuhi ya kikanivali, kitashtiti, maadili, mawazo, ucheshi na zimbwe. Mifano mizuri ya futuhi ni ‘Aliyeonja Pepo’ (Topan, F.), ‘Usaliti Mjini’ (Imbuga, F.), Twelfth Night (Shakespeare, W.), Importance of Being Earnest (Wilde Oscar), Mkaguzi Mkuu wa Serikali (Gogol, Nikolai), The Lion and the Jewel (Soyinka, W.) na ‘Masaibu ya Ndugu Jero’ (Soyinka, W.).
MELODRAMA
Katika zama za urasimi, aina hii ilitumiwa kuelezea aina ya drama au tamthiliya iliyokuwa na matumizi mengi ya uimbaji au nyimbo (melos). Kwa hiyo, melodrama ni dhana inayotumiwa kuelezea aina ya tamthiliya ambayo imetawaliwa na uimbaji wa nyimbo.
Melodrama inafanana sana na tanzia ingawa mara nyingi nguli wa melodrama humalizika na ushindi, matokeo yake yanasisimua sana na mwendo wa msuko wake huwa ni wa haraka haraka zaidi. Wahusika wake huvutia na kufurahisha lakini hawana sifa za kishujaa.
Dhamira ya melodrama huzungukia mvutano kati ya wema na uovu au ubaya. Miishio ya tamthiliya hizi haina sifa ya mtakasohisia kama ilivyo na tanzia bali huwa ni aina ya ushindi wa mhusika mwema. Mfano mzuri ni ‘The Begger’s Opera’ iliyotungwa na mwanatamthiliya wa Kiingereza John Gay kunako 1728.
 TANZIA-RAMSA
Ni tamthiliya inayochanganya vipengele vya tanzia na ramsa, hutumiwa sawa na tamthiliya za kibwege - hii ni tamthiliya ambayoinaonyesha kwamba kicheko au furaha ndiyo jibu pekee la maisha kwa watu ambao hawana imani na maisha ambayo kwayo misingi thabiti ya maisha imeondolewa. Mfano tamthiliya ya  Amezidi ya S.A Mohamedi
Tanzia-ramsa ni aina huonyesha mabadiliko ya aina fulani yanayogeuza mwelekeo wa matukio ya kitanzia na kuufanya kuwa tofauti au wa kufurahisha. Hali hii inaweza kupatikana kwa kuwepo kwa hasidi au mui anayetubu na kuyajutia makosa au msimamo wake au kuwepo kwa mandhari ya kiulimbwende.
Kimsingi, tanzia-ramsa ni tanzia inayoishia kwa furaha. Kinyume chake ni futuhi zimbwe. Dhana hii inaakisi kwa kiasi kikubwa baadhi ya mitazamo ya kidhanaishi ya fasihi ambapo ushujaa na tanzia havijitokezi katika hali ya kawaida kama vilivyozoeleka.
Hali hii inadhihirika katika tamthiliya kama vile ‘The Cherry Orchard’ (Anton Chekhov, 1904), ‘The Winter’s Tale’ (William Shakespeare, 1611).
FUTUHI/KOMEDIA (COMEDY)
Futuhi au komedia ni utungo ambao unachekesha na kuchangamsha. Tamthiliya ya aina hii inaweza kusawiria picha yakini katika maisha  kwa undani ikitumia dhihaka na kejeli kwa kuchekesha. Futuhi huficha ukali wa masuto kadri inavyoendelea kuburudisha hadhira yake.
Futuhi hulenga kurekebisha tabia inazozidhihaki au inazozicheka. Kusema futuhi inafurahisha haina maana kuwa dhamira yake haina uzito. Futuhi huzungumzia masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa njia ya kuchekesha. Futuhi huweza kuwa na sifa zinazotofautiana – jambo ambalo hutumiwa kama kigezo cha kuainisha aina mbalimbali. Lakini vyovyote iwavyo, futuhi hujikwepesha na masuala ya kutia hofu au kushtua.
Athari ya futuhi (kuchekesha) hutokana na matendo, mienendo ya wahusika na hitilafu au ila za kuingiliana kwa kiusemi. Futuhi huwa na viwango mbalimbali vya kuchekesha.
Kwanza, kuna kiwango hafifu (duni) ambacho huhusishwa na futuhi ya chini. Kuna baadhi ya kazi ambapo kiwango cha kuchekesha huwa kigumu kutambulikana na huhitaji utambuzi mpevu. Hii ni sifa ya aina ya futuhi iitwayo Futuhi ya Juu.
Aina zingine ni pamoja na, futuhi ya kikanivali, kitashtiti, maadili, mawazo, ucheshi na zimbwe. Mifano mizuri ya futuhi ni ‘Aliyeonja Pepo’ (Topan, F.), ‘Usaliti Mjini’ (Imbuga, F.), Twelfth Night (Shakespeare, W.), Importance of Being Earnest (Wilde Oscar), Mkaguzi Mkuu wa Serikali (Gogol, Nikolai), The Lion and the Jewel (Soyinka, W.) na ‘Masaibu ya Ndugu Jero’ (Soyinka, W.).
MELODRAMA
Katika zama za urasimi, aina hii ilitumiwa kuelezea aina ya drama au tamthiliya iliyokuwa na matumizi mengi ya uimbaji au nyimbo (melos). Kwa hiyo, melodrama ni dhana inayotumiwa kuelezea aina ya tamthiliya ambayo imetawaliwa na uimbaji wa nyimbo.
Melodrama inafanana sana na tanzia ingawa mara nyingi nguli wa melodrama humalizika na ushindi, matokeo yake yanasisimua sana na mwendo wa msuko wake huwa ni wa haraka haraka zaidi. Wahusika wake huvutia na kufurahisha lakini hawana sifa za kishujaa.
Dhamira ya melodrama huzungukia mvutano kati ya wema na uovu au ubaya. Miishio ya tamthiliya hizi haina sifa ya mtakasohisia kama ilivyo na tanzia bali huwa ni aina ya ushindi wa mhusika mwema. Mfano mzuri ni ‘The Begger’s Opera’ iliyotungwa na mwanatamthiliya wa Kiingereza John Gay kunako 1728.

2. RAMSA/KOMEDI
 Ni tamthiliya ambayo inachangamsha na huishia kwa kufurahisha na ni ya vichekesho, hii haina maana kwamba haina maudhui mazito ndani yake.
 Inashughulikia mambo yale yale yanayoweza kushughulikiwa na tanzia. Mfano masuala ya unafiki,uzembe, wivu, hivyo inayashughulikia kwa namna tofauti na tanzia
Udhati wa ramsa si kwamba usanii humalizika katika kicheko/furaha zaidi ni kuishia mhusika mkuu kufanikiwa
Shujaa wa kiramsa
·        Si lazima awe mtu maalum/mbabe au shujaa, anaweza kuwa mtu wa kawaida
·        Mhusika wa ramsa lazima awe mtu wa wastani chini ya wastani, awe ni mtu ambaye hatarajiwi kujitokeza na mtu wa nasaba duni na matendo yake yawe ya ucheshi
·        Ni lazima awe mtu ambaye akifanikiwa wasomaji au watazamaji watafurahi
Uhusika katika ramsa
·        Ramsa inawahusu watu wa kawaida kuliko ilivyo tanzia
·        Inawahusu watu wa kipato cha kati na cha chini
·        Dhamira zote huelekezwa kwa watu wa kipato cha chini na duni. Mfano walalahoi
 SIFA ZA RAMSA
·        Sharti ivutie akili na siyo hisia
·        Ni lazima kuwa na matendo bila kufikiria hii itapelekea msomaji au mtazamaji kujua kwamba wahusika hawa hawana akili
·        Lazima iwe na hali ya utu (ikitukumbusha ubinadamu wetu)
·        Sharti iwe na mila na desturi ambazo hadhira inazifahamu toka katika jamii yake
·        Hadhira isiogope au kupata uchungu kwa sababu hii sio lengo lengo la ramsa
·        Wahusika wa ramsa hujaribu kuepuka vikwazo ambavyo vimewekwa
·        Inaonyesha haja ya kuikomboa nafsi Mfano wa ramsa ni kama vile Mfalme Juha.


MAREJELEO
Muhando,P. (1982), Lina Ubani, Dar es Salaam University Press: Dar es Salaam.
Wamitila, K.W. (2003), Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi. English press: Nairobi
Senkoro, F. E. M. K. (2006), Kioo cha Lugha, Fasihi ya Kiswahili ya Majaribio; Juzuu namba (4) TUKI: Dar es Salaam. 

NB; Makosa ya kitahajia au kimaana yaliyojitokeza katika makala hii, ni makosa ya kiuchapaji hivyo hayahusiani na vyanzo rejelezi vilivyooneshwa hapo juu.



Maoni 4 :

  1. kwa ujumla hii makala nimeipenda sana maana imeelezea vizuri sana
    nina swali pia,
    toa maana ya tamthiliya ya majaribio na ujadili vipengele vyake.

    JibuFuta
  2. shukrani kwa nakala yako nzuri

    JibuFuta
  3. makala ya maana zaidi, heko.

    JibuFuta